MSEMAJI Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amesema kazi ya uandishi wa habari hapa nchini inasimamiwa na sheria ya huduma za vyombo vya habari sura namba 229,na kwamba hakuna mtu anayeruhusiwa kutumia vyombo vya habari kwa maslahi yake binafsi
Akizungumza katika kongamano la maadhimisho ya miaka 30 ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani mjini Unguja, Msigwa amesema kuna baadhi ya watu wamekuwa wakifanya mzaha na tasnia ya habari, jambo ambalo halitavumiliwa.
“ Tasnia ya uandishi wa habari haifungi milango kwamba mtu mwingine haruhusiwi kwenda, muhimu ni kuzingatia maadili ya uandishi, miiko ya uandishi wa habari misingi ya uandishi wa habari, tunachotoa wito kwao waende kwenye vyuo vipo watasoma watapandikizwa taaluma,” alisema Msigwa.
Kuhusu ulinzi wa waandishi wa habar, Msigwa amesema serikali haijawahi kufumbia macho ulinzi wa vyombo vya habari nchini.
Hatahivyo amewaon ya wamiliki wa vyombo ambao wanakataa kuwaajiri waandishi wa habari wanawake na kusema ni kosa la kisheria.
“ Ni vizuri waandishi wa habari wanawake wakatambua kwamba wanapofanya kazi hii si suala la kazi yake la ajira yake tu, lakini ajue kwamba amebeba majukumu zaidi ya kusimamia mambo mengi ya wanawake ambao sio waandishi wa habari, kwa hiyo ni kazi ambayo mimi nasema ni wito na waandishi wa habari wanawake naona agenda za wanawake zina watu wa kuzisukuma,” alifafanua Msigwa.
Kongamano hilo linataraji kufikia kielle chake hii leo Mei 3, 2022, ambapo Tanzania inaungana na nchi nyingine duniani kuadhimisha siku ya uhuru wa vyombo vya habari duniani.