Wenye ulemavu watakiwa kuchangamkia fursa

Profesa Joyce Ndalichako

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Profesa Joyce Ndalichako amewataka watu wenye ulemavu kuchangamkia fursa ambazo Serikali inazitengeneza ikiwemo fursa za ajira.

Profesa Ndalichako alitoa rai hiyo Jumatatu wakati wa kuzindua Baraza la Ushauri la Taifa kwa Watu wenye Ulemavu.

Alisema Serikali imekuwa ikitoa fursa nyingi ambazo watu wenye ulemavu wanahaki ya kushiriki na kuwataka kuchangamkia kila fursa inayotolewa.

Advertisement

Akifafanua zaidi, Profesa Ndalichako alisema Serikali imeweka sheria ambayo inawataka waajiri katika sekta ya umma na binafsi kutoa asilimia tatu ya ajira zinazotangazwa kwa watu wenye ulemavu lakini watu wa kundi hilo wamekuwa hawajitokezi ipasavyo.

Alisema pia Serikali kupitia Ofisi ya Wa

ziri Mkuu imekuwa ikitenga fedha kwa ajili ya kuwainua wananchi kiuchumi, kukuza ujuzi lakini mwamko wa watu wenye ulemavu kushiriki katika fursa hizo umekuwa mdogo sana.

“Mfano kwa mwaka wa fedha 2022/23 Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu imetenga shilingi bilioni 9, lakini ukienda kwenye utekelezaji hatuwaoni vijana wenye ulemavu kuchangamkia fursa hii.”

Kutokana na hali hiyo, Profesa Ndalichako alimuagiza Katibu Mkuu, Profesa Jamal Katundu kuweka mfumo mzuri wa mawasiliano na vyama vya watu wenye ulemavu ili fursa zinapotolewa basi taarifa ziweze kufika kwa walengwa.

Naye Mwenyekiti wa Baraza hilo, Dk Lucas Kija pamoja na kushukuru kwa uteuzi aliomba Serikali kuharakisha mchakato wa uanzishwaji wa Mfuko wa Walemavu.

Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Profesa Jamal Katundu alisema Baraza hilo litadumu kwa miaka mitatu.

Akitoa salamu za wadau wa maendeleo, Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Christian Blind Mission, Nensia Mahenge alisema wadau wa maendeleo watashirikiana na baraza hilo katika kuhakikisha haki za watu wenye ulemavu zinazingatiwa.

 

 

 

/* */