Wenye VVU wanaweza kuwa na afya, furaha

UJUMBE uliotolewa na zaidi ya wanawake watano wa mjini Iringa wanaoishi na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) kwa zaidi ya miaka 10, umeonesha, licha ya changamoto wanazopata, watu wengi wenye maambukizi hayo wana uwezo wa kuishi maisha yenye afya na furaha.

Kwa mujibu wa utafiti wa viashiria na matokeo ya UKIMWI wa mwaka 2016/2017 mkoa Iringa ni moja ya mikoa iliyoathiriwa sana na maambukizi hayo lakini kwa kupitia juhudi za serikali na mashirika ya kimataifa, mchango mkubwa unatolewa katika kuimarisha afya na kuleta furaha kwa watu wanaoishi na VVU (WAVIU).

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Halima Dendego anasema asilimia 11.3 ya watu zaidi ya Milioni 1.92 mkoani mwake wanakadiriwa kuwa na VVU na kuufanya mkoa huo kuwa wa pili kitaifa kwa maambukizi hayo baada ya mkoa wa Njombe wenye asilimia 11.4.

Kati ya wanawake hao watano, mmoja wao ni mwanafunzi wa vyuo vikuu vya Kusini aliyejitambulisha kwa jina moja la Lucy akisema; “Nilijulikana na maambukizi ya VVU mwaka 2013 na wakati huo nikiwa na miaka 12, nilikuwa na hofu ya kifo lakini elimu na mafunzo yamenipa afya na furaha mpaka leo hii.”

Lucy na wanawake wenzie wenye VVU walitoa ujumbe wao kwa Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) Craig Hart, wanahabari pamoja na wawakilishi wa mashirika mbalimbali yanayotekeleza miradi ya Ukimwi nchini inayofadhiliwa na Mfuko wa Dharula wa Rais wa Marekani wa Kukabiliana na Ukimwi (PEPFAR) kupitia USAID.

“Toka wakati huo hadi sasa nimepitia changamoto mbalimbali; nimetafsiriwa kama msichana malaya pamoja na kwamba mimi sikupata maambukizi kwa kupitia tendo la ndoa, nimetengwa, nimebaguliwa na nimesimangwa na kutolewa kila aina ya mfano wa wanawake wabaya kwasababu tu nina maambukizi haya,” anasema Lucy.

Kwa kupitia mradi wa USAID Boresha Afya, Lucy anaushukuru Mfuko wa PEPFAR kwa kuwawezesha wenye maambukizi kama yeye kupata dawa za kufubaza makali ya VVU (ARVs), elimu na kupunguza unyanyapaa, chakula, uhamasishaji wa huduma za afya na ufuatiliaji na rasilimali fedha.

“Mafunzo niliyopata kupitia mradi huo yameniwezesha kuondokana na dhana potofu na unyanyapaa, uelewa na kuhamasisha jamii kuhusu kuheshimu haki za watu wanaoishi na VVU na kusaidia juhudi za kuzuia maambukizi mapya, kushughulikia changamoto za kihisia na kijamii tunazokutana nazo, kutangaza hali yangu na kushiriki katika shughuli za kijamii bila kuogopa unyanyapaa na ubaguzi, na kuwa na sauti yenye nguvu katika jamii,” anasema.

Yote hayo anasema yamemuwezesha kuchaguliwa kuwa mwakilishi wa vijana wanaoishi na VVU Mkoa wa Iringa lakini pia mapema mwaka huu alichaguliwa kuwawakilisha wasichana wanaoishi na VVU Tanzania katika Mkutano wa United! Youth Leadership Summit uliofanyika Afrika Kusini na kujadili masuala ya afya ya uzazi na Ukimwi kwa vijana wa miaka 15 na 24.

Lucy anakosoa mafunzo na elimu kwa vijana wa vyuo vikuu akisema katika baadhi ya maeneo, elimu ya Ukimwi vyuoni bado haitoshi au inahitaji kuboreshwa ili kukuza tabia nzuri za kujilinda na kupunguza unyanyapaa.

Mkurugenzi Mkazi wa USAID anasema; “Tunaadhimisha miaka 20 ya PEPFAR tukishuhudia zaidi ya watanzania Milioni 1.5 ambao ni sawa na asilimia 98 ya watanzania wote wanaoishi na VVU wakinufaika na Mfuko huu ulioanzishwa na Rais George W. Bush Mwaka 2003 ukiwa na jukumu kubwa katika kutoa msaada wa kifedha na kiufundi kwa nchi nyingi ili kupunguza maambukizi ya VVU, kutoa matibabu na kusaidia wale wanaoishi na VVU/Ukimwi.”

Hart anasema PEPFAR kwa kupitia miradi mbalimbali ambayo ufadhili wake unapitia USAID imetoa mchango mkubwa katika kuhakikisha upatikanaji wa dawa za kupunguza makali ya VVV (ARVs) na hivyo kusaidia kuongeza muda wa maisha na kuimarisha afya ya watanzania wengi na inazingatia kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto kupitia huduma za PMTCT.

Anasema PEPFAR pia inaendesha kampeni za uhamasishaji na elimu kuhusu VVU/Ukimwi ili kuongeza uelewa katika jamii na kupunguza unyanyapaa, na imechangia katika uimarishaji wa miundombinu ya afya pamoja na kutoa mafunzo kwa watoa huduma za afya, kuboresha vituo vya kutolea huduma za afya na upatikanaji wa vifaa muhimu.

Aidha anasema PEPFAR imesaidia kutoa msaada wa kisaikolojia na kijamii kwa watu wanaoishi na VVU hiyo ikiwa ni pamoja na huduma za ushauri nasaha, vikundi vya msaada na mifumo inayosaidia ustawi wa kijamii.

“Mfuko huu pia umekuwa ukijitahidi kuwajumuisha watu wanaoishi na VVU katika maamuzi yanayowahusu na kuwawezesha kuchangia juhudi za kupambana na Ukimwi. Lakini pia PAPFAR imekuwa ikiunga mkono miradi ya utafiti inayolenga kuboresha matibabu, kuelewa zaidi virusi vya Ukimwi vinavyoenea na kubuni mikakati bora ya kuzuia maambukizi ya VVU,” anasema.

Anasema misaada yao kwa watu wa Tanzania ni uwekezaji usioepukika kwa kutambua kwamba theluthi mbili ya idadi ya watu wake ni vijana ambao ni kizazi cha sasa na kijacho.

Akizungumzia mafanikio ya mfuko huo, Hart amesema toka mwaka 2003 Serikali ya Watu wa Marekani imetoa zaidi ya Dola za Kimarekeni Bilioni 6 ikiwa ni pamoja na Dola Milioni 450 kwa mwaka 2022 pekee kupitia miradi mbalimbali ya kupambana na ugonjwa wa Ukimwi nchini Tanzania.

Miradi hiyo ni pamoja na USAID Afya Yangu Kanda ya Kusini unaolenga utoaji huduma jumuishi za matunzo, matibabu na kuzuia maambukizi ya VVU na Kifua Kikuu na kuboresha mazingira wezeshi ya utoaji wa huduma bora za afya katika mikoa sita ya kusini mwa Tanzania.

Mradi mwingine ni USAID Kizazi Hodari Kusini unaongalia utoaji wa huduma jumuishi za watoto yatima na wanaoishi katika mazingira hatarishi pamoja na walezi wao ili kuboresha afya, ustawi na ulinzi wa watoto hao pamoja na vijana wa mikoa 11 kupitia shirika la Deloitte.

Mwingine ni mradi wa Epic unaotekelezwa na Shirika FHI360 ukijikita katika kufikia na kuendeleza udhibiti wa janga la VVU na kutoa msaada wa kitaalamu na huduma za moja kwa moja ili kuondoa vikwazo katika kufikia malengo ya 95-95-95 kwa kulenga makundi maalumu wakiwemo wasichana, wamama vijana, wanaume na wanawake walio katika hatari ya kupata maambukizi ya VVU.

Malengo ya 95-95-95 yanalenga asilimia 95 ya watu wote wanaoishi na VVU wanajua hali zao, asilimia 95 ya wale wanaojua hali zao wanapata matibabu ya kupunguza makali ya VVU na hatimaye asilimia 95 kati yao wanafikia kiwango cha chini cha VVU mwilini.

Mradi mwingine unaotekelezwa na Baraza la Taifa la Watu Wanaoishi na VVU Tanzania (NACOPHA) wa Hebu Tuyajenge unashirikisha watu wanaoishi na VVU ukilenga katika kuongeza matumizi ya huduma za upimaji wa VVU, tiba na uzazi wa mpango miongoni mwa vijana balee na wenye VVU.

Mratibu wa Mfuko wa PEPFAR nchini, Jessica Greene ameupongeza mkoa wa Iringa kwa kuwa moja ya mikoa inayomufaika na miradi hiyo akisema juhudi hizo zinachangia kwa kiasi kikubwa katika kupunguza athari za Ukimwi na zinaonesha jukumu muhimu la ushirikiano wa kimataifa katika kukabiliana na janga hilo.

“Tumeungana na serikali ya Tanzania katika kuhakikisha vipaumbele hivyo vinafanikiwa na tutaendelea kuhakikisha watu wenye VVU wanapata huduma bora, matunzo na tiba,” amesema.

Greene amesema kwa watu wenye VVU, kuwa na afya njema na kujisikia furaha ni muhimu siyo tu kwa maisha yao ya kila siku pia kwa mchakato wa matibabu na ustawi wao kijamii.

Habari Zifananazo

Back to top button