Wenyeviti vijiji waliouza ardhi kiholela matatani

Wenyeviti vijiji waliouza ardhi kiholela matatani

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kigoma kimetoa maelekezo kwa ofisi ya Mkuu wa Wilaya Uvinza na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo kuwakamata na kuwafungulia mashitaka viongozi wa vijiji waliouza maeneo ya vijiji vyao kinyume cha sheria.

Katibu wa CCM Mkoa Kigoma, Mobutu Malima alitoa maelekezo hayo wakati akizungumza kwenye mkutano na viongozi wa vijiji, wenyeviti na makatibu wa kata za wilaya ya Uvinza na kubainisha kuwa matendo yaliyofanywa na viongozi hao wa vijiji hayakubaliki.

Katika mkutano huo ulihudhuriwa na wenyeviti wa vijiji 45 kati ya vijiji 61 vilivyopo kwenye wilaya hiyo.

Advertisement

Malima alitoa maelekezo kukamatwa na kuchukuliwa hatua kwa wenyeviti wa vijiji vitano ambao wamekuwa vinara wa uuzwaji wa maeneo kwenye vijiji vyao kwa kukiuka sheria.

Alivitaja vijiji hivyo kuwa ni pamoja na Mgambazi, Chakuru, Rukoma, Lufubu na Malagarasi ambapo wenyeviti hao wanadaiwa kuuza hadi hekta 1,000 kwa mtu mmoja wakati sheria haiwapi mamlaka hayo.

Akizungumza katika kikao cha ndani kilichohudhuriwa na wajumbe wa kamati ya siasa ya Wilaya ya Uvinza Mwenyekiti wa CCM wa wilaya hiyo, Emanuel Kalayenga alisema alifanya ziara na kamati ya siasa ya wilaya na kushuhudia changamoto ya matumizi mabaya ya madaraka ya viongozi wa vijiji wengi wakilalamikiwa kwa ubabe, jeuri na kujichukulia sheria bila kufuata taratibu.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Uvinza, Masumbuko Kechegwa alisema kuwa tayari hatua zimeanza kuchukuliwa ikiwemo kusimamishwa kwa wenyeviti wa vijiji ikiwemo Kijiji cha Lufubu ambapo mwenyekiti wake anatuhumiwa kuuza eneo lenye ukubwa wa zaidi ya hekta 1,000.