Wenza wafundwa mgawo wa mali wakiachana

CHAMA cha Wanasheria Wanawake (TAWLA) na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), wametoa ushauri kwa watu wafunge ndoa ili kuepuka migogoro ya mali na matunzo ya watoto wanapoachana.

“Sheria inataka watu wawili walioishi pamoja muda mrefu waende mahakamani kupeleka vithibitisho ambapo mahakama sasa ndio itatamka kama hiyo ni ndoa ama la ndio masuala mengine yaendelee,” alisema Mkurugenzi Mtendaji wa Tawla, Tike Mwambipile.

Mwambipile alisema mlolongo unakuwa mrefu ikitokea wawili hao kufarakana hivyo ili kuepuka hayo anashauri wahusika wenye uhusiano wa kimapenzi wafunge ndoa.

“Sasa si unaona mpaka sijui majirani, ndugu wapeleke vithibitisho mahakamani kwamba ninyi mmeishi pamoja muda fulani na mahakama itamke kuitambua kama ndoa, sasa hayo yote ya nini? Kuhusu watoto waishi na nani hilo halina shida kwa sababu siku hizi wanatizama ustawi…nashauri wafunge ndoa changamoto ni nyingi kuishi bila ndoa,” alieleza.

Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Anna Henga alisema ni muhimu wenza wafunge ndoa ili kupata haki kwa urahisi.

“Kuishi zaidi ya miaka miwili ni dhana ya ndoa kifungu namba 160, hii inatokea pale unapokuta kuna mali zimechumwa pamoja…dhana ya ndoa sio ndoa, ndoa ni ile iliyosajiliwa na kufungwa kulingana na utaratibu uliowekwa kisheria. Mtu aliye kwenye dhana ya ndoa ana hatari zaidi ya kupoteza haki yake kuliko kuipata,” alisema Henga.

Alisema watoto baada ya wazazi walio kwenye dhana ya ndoa kutengana, wana haki ya kutunzwa na mali za wazazi wao na hawana haki katika mgawo wa wazazi wao ila watakuwa na haki ya kurithi endapo wazazi watafariki.

Wakili wa Serikali, Gloria Msyulila alisema kwa mujibu wa sheria ya ndoa ya Tanzania, ikithibitika kuwa mwanamume na mwanamke wameishi pamoja kwa miaka miwili au zaidi katika hadhi ya mume na mke, basi kutakuwa na dhana ya ndoa.

Msyulila alisema ili mtu aishawishi mahakama kuhusu dhana ya ndoa inabidi athibitishe kuwa ziwe ni jinsi mbili yaani ya kiume na ya kike kwa kuwa Tanzania haitambui ndoa za jinsi moja.

“Inahitaji kuthibitika kuwa watu hawa huwa wanaishi katika nyumba moja kama mke na mume, hivyo kutembelewa na mpenzi wako kwa kipindi kifupi kama wikiendi na kukaa pamoja kisha kila mtu anarudi kwake haiwezi kutumika kuthibitisha dhana ya ndoa,” alisema Msyulila.

Wakili wa Kujitegemea, Aliko Mwamanenge alisema wakati wa mgawanyo wa mali ni lazima kuwe na ushahidi utakaodhihirisha pasipo kuacha shaka kuwa mhusika alichangia katika kuzipata.

“Mfano kama mume alikuwa na mali zake kabla ya kuwa na huyo mke wakati wa kugawana mali hawatagawana mali hizo, watagawana zile walizotafuta wakiwa wote,” alisema Mwamanenge.

Alisema ili wawe wameishi katika hadhi ya mume na mke ni lazima pathibitike kuwa wawili hao wameishi katika hali ya kuwapa hadhi ya mke na mume, mfano kuzaa na kuwapo na majirani watakaokuwa mashahidi.

Wakili Innocent Shayo alisema wakati wa mgawanyo wa mali kwa upande wa mwanamke, hata kama hakuchangia fedha au kitu kingine utazingatiwa mchango wake akiwa mke likiwamo tendo la ndoa, kulea watoto, kumpikia mumewe, kumfulia nk.

Kwa upande wa mchango wa wanaume, alisema mahakama itaangalia kama walinunua vitu pamoja iwe gari au nyumba watagawana kwa asilimia 50 kwa 50.

“Kama mmojawapo aliitafuta mali mwenyewe na akamuandikisha mtoto ambaye si wa ndoa yao basi hizo mali hazitagawanywa kwa wote itabaki kuwa mali ya mtoto,” alisema Shayo.

Aliongeza: “Kama watu hao waliishi chini ya miaka miwili hao si wanandoa hata kama kuna mali walizipata wakiwa pamoja na kama ikitokea wametengana basi shauri lao litafunguliwa mahakama kama shauri la madai ya kawaida na si kama wanandoa.”

Habari Zifananazo

Back to top button