DODOMA: MBUNGE wa Mbogwe, Nicodemas Maganga amemueleza Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Tulia Ackson kuwa wabunge wamekubaliana kuwasilisha sheria ya kunyongwa kwa yeyote ambae atabainika kuiba fedha za umma.
Akizungumza leo Novemba 4, 2023 Maganga amesema mpaka jana wamefikia Wabunge 168 ambao wamekubaliana kwa pamoja kushughulikia mpango wa kupeleka sheria hiyo.
“Sheria tutakayoleta itaruhusu wezi wa fedha za umma kunyongwa tumefikia hatua hii kwa kuwa watu wamekuwa wagumu kuelewa na hata wakipelekwa Mahakama na kutozwa faini imekuwa haitoshi kuwa kama adhabu kwa makosa hayo.”Amesema
Hoja ya kupeleka Bungeni sheria ya wezi za fedha za umma kunyongwa ilianza kuibuliwa jana na mbunge wa Tarime vijijini, Mwita Waitara ambaye aliungwa mkono na baadhi ya Wabunge waliposimama kuchangia hoja zao.
Bunge linaendelea na mjadala wa taarifa za Kamati tatu za bunge kuhusu ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).