JE, unajua kuwa unatakiwa unywe kiasi cha lita 200 za maziwa kwa mwaka?
Wakati Shirika la Afya Duniani (WHO) likipendekeza kila mtu kunywa kiasi cha lita 200 za maziwa kwa mwaka, hapa Tanzania hali ni tofauti.
Kwa mujibu wa Msajili wa Bodi ya maziwa nchini, Dk George Mutani, takwimu zinaonesha kuwa kila mtanzania anatumia kiasi cha kita 62 tu za maziwa kwa mwaka.
Akizungumza katika maadhimisho ya wiki ya maziwa yaliyofanyika jijini Dodoma, msajili wa Bodi ya Maziwa alisema kuwa Tanzania huzalisha lita bilioni 3.4 za maziwa kwa mwaka huku wastani wa unywaji maziwa ukiwa bado chini.
Pamoja na kuwataka Watanzania kunywa maziwa kwa wingi, ameshauri: “Tuwape watoto maziwa ili wakue vizuri. Tafiti zinaonesha watoto wanaokunywa maziwa wanafanya vizuri katika masomo yao.”
Alisema kuwa maziwa ni chakula cha msingi kwa watoto na watu wazima kuhakikisha wanakunywa maziwa bila kukosa.
“Tusiache kunywa maziwa, tunywe maziwa salama ambayo ni yale yaliyosindikwa kwa ubora,” amesisitiza.
Alisema kuwa mpango wa unywaji maziwa shuleni ulianzishwa mwaka 2000 na wadau wa maziwa. Kwa Uratibu wa Shirika la Chakula Duniani (FAO).
Katika kuhamasisha zoezi hilo, maadhimisho hayo yalienda sambamba na ugawaji wa maziwa kwenye shule zenye wanafunzi wenye mahitaji maalum za Nkuhungu, Chinangali, Mlezi na Dodoma Viziwi.
Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo Mwenyekiti wa Bodi ya Maziwa Tanzania, Zacharia Masanjiwa amesema kuwa unywaji maziwa shuleni unatakiwa kuwa endelevu ili kuboresha afya na akili za watoto.
Naye Kaimu Meneja Masoko wa bodi hiyo, Joseph Semu alisema kuwa katika maadhimisho hayo, ugawaji wa maziwa kwa shule hizo umefanikishwa na kampuni za kusindika maziwa za Asasi, Dodoma Halisi na Tanga Fresh.
Kwa upande wake, Ofisa Lishe kutoka Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) amesema kuwa Shirika hilo na Tanzania kupitia programu inayofadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU) inayoitwa AGRI-CONNECT, zimezindua kampeni ya kitaifa ya lishe ili kuhamasisha ulaji sasa.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Dodoma Viziwi, Kennedy Maingu alisema kuwa Shule hiyo ina wanafunzi 130 na Walimu 24 na kuiomba Serikali iongeze bajeti ya chakula.