WHO, Unicef yasifu serikali utoaji chanjo
WAZIRI wa Afya, Ummy Mwalimu amesema serikali inathamini mchango unaotolewa na mashirika ya kimataifa kwenye maendeleo ya sekta ya afya nchini.
Ummy aliyasema hayo juzi jijini Dar es Salaam alipokutana na kufanya mazungumzo na Kaimu Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) nchini, Dk Zabron Yoti pamoja na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Watoto (UNICEF) nchini, Shalini Bahuguna.
“Serikali itaendelea kufanya kazi na Who, Unicef pamoja na mashirika mengine ya ndani na nje ya nchi kwa manufaa ya ustawi wa afya za Watanzania,” alisema. Ummy alipongeza jitihada zinazofanywa na wadau hao wa maendeleo katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Covid-19 kwa kutoa rasilimali pamoja na kujikita katika utoaji wa elimu na hamasa ya chanjo dhidi ya ugonjwa huo.
Katika kikao hicho, viongozi hao pia walijadili kuhusu utoaji wa chanjo aina mbalimbali za watoto ikiwamo ya polio kwa awamu ya tatu inayotarajiwa kufanyika hivi karibuni. Kwa upande wao wadau hao wa maendeleo, waliipongeza serikali kwa jitihada inazozifanya kuhamasisha na kutoa elimu ya chanjo dhidi ya Covid-19.
Dk Yoti aliihakikishia serikali kuwa Who itaendelea kuwa mshirika wa karibu zaidi na kutoa msaada wa kitaaluma na rasilimali katika kusaidia serikali kupambana na majanga ya magonjwa mbalimbali. Bahuguna alisema ameshuhudia wingi wa wananchi wakihamasika na kujitokeza kupata chanjo dhidi ya Covid-19.
Alipongeza mkakati wa wizara pamoja na wadau wengine kutumia watu wenye ushawishi ndani ya jamii kuhamasisha wananchi kujitokeza kupata chanjo.