SHIRIKA la Afya Duniani (WHO) limeitaja Tanzania kuwa miongoni mwa nchi ambazo zimevuka au kufikia lengo la kupunguza maambukizi mapya ya kifua kikuu (TB) ndani ya muongo mmoja.
Katika ujumbe wake wa Siku ya Kifua Kikuu Duniani iliyoadhimishwa jana mkoani Simiyu, Mkurugenzi wa WHO Kanda ya Afrika, Dk Matshidiso Moeti alitaja nchi nyingine kuwa ni Ethiopia, Kenya, Lesotho, Namibia, Afrika Kusini na Zambia.
Alisema zimevuka au kufikia lengo la asilimia 20 la kupunguza wagonjwa wapya kutokana na msaada wa kiufundi, uraghibishi na ushirikiano endelevu kutoka WHO.
“Maendeleo makubwa yamepatikana katika muongo mmoja uliopita, hasa katika Kanda za Afrika Mashariki na Kusini. Nchi zenye mzigo mkubwa, kama vile Tanzania… zimevuka au kufikia lengo la asilimia 20 la kupunguza visa vipya vya TB,” alisema.
Dk Moeti alisihi viongozi, serikali, washirika wa maendeleao, jamii na wadau wote kuendeleza kwa haraka mifumo thabiti ya afya inayohitajika ili kufikia malengo ya Maendeleo Endelevu ifikapo mwaka 2030.
Kuhusu maadhimisho ya Siku ya Kifua Kikuu Duniani ambayo hufanyika kila Machi 24, alisema lengo ni kuhamasisha umma kujikinga, kufahamu athari za kiafya, kijamii na kiuchumi zitokanazo na ugonjwa huo unaozuilika. Kauli mbiu ya mwaka huu ni ‘Ndiyo, tunaweza kukomesha TB.’
Aidha, akizungumza katika maadhimisho hayo mjini Bariadi, Dk Johnson Lyimo kutoka WHO Tanzania, alipongeza uzinduzi wa mpango wa kisekta kati ya serikali na wadau uliofanyika jana ambao lengo lake ni kuweka mkakati wa kisekta wa kukabili ugonjwa huu nje ya sekta ya afya.
“Sisi tumekuwa tukijaribu kushauri mapambano lazima yakabiliwe kisekta zaidi ya sekta ya afya maana wanaokabiliwa na TB ni watu wenye umasikini, matatizo ya kiuchumi…ili kutatua hivi vitu, ni lazima kuwe na mkakati wa kisekta,” alisema.
Alisema WHO imekuwa ikishirikiana na serikali na wadau kutengeneza mkakati wa nchi ambao amesema ni jambo la kupongeza kuona umekamilika. “Leo tumefikia mwisho wa hii hatua, tumezindua huu mfumo kushirikisha serikali na wadau wengine nje ya sekta ya afya.
Kwa mujibu wa Dk Lyimo, mpango huo uliidhinishwa mwaka 2017 katika mkutano wa WHO baada ya kudhihirika kuwa panahitaji mkakati nje ya sekta ya afya.
Mwenyekiti wa Muungano wa Wadau wanaohusika na kutokomeza Kifua Kikuu Tanzania (Stop TB), Dk Peter Bujari alisema panahitajika wadau kushirikiana kutokomeza ugonjwa huo na si kuachia Wizara ya Afya pekee.
Awali, katika ujumbe wake, Dk Moeti alisema WHO inafurahi kuona nchi wanachama zinaongeza matumizi ya zana na mwongozo mpya unaopendekezwa na shirika na hivyo kupanua wigo wa huduma