WHO yatoa msaada dawa kutibu maji

SHIRIKA la Afya la Umoja wa Mataifa (WHO),  limekabidhi kwa idara ya afya Mkoa Kigoma dawa na vifaa mbalimbali kwa ajili ya kuzuia magonjwa yatokanayo na uchafuzi wa maji ikiwemo kipindipindu na ugonjwa wa matumbo.

Mwakilishi wa WHO Mkoa Kigoma, Jairos Hiliza alikabidhi misaada hiyo kwa Mganga Mkuu wa Mkoa Kigoma,Dk Jesca Lebba kwa niaba ya waganga wakuu wa halmashauri tisa za mkoa Kigoma ambako zitagawanywa.

Miongoni mwa misaada iliyotolewa ni pamoja na boksi 50 za dawa za vidonge vya kutibu maji. vifaa vya kupima kiwango na ubora wa maji 100, vitakasa mikono 42 na vipeperushi 1000 kwa ajili ya kutawanywa kwenye shule mbalimbali mkoani Kigoma.

Akikabidhi misaada hiyo Mwakilishi huyo wa WHO alisema kuwa imetolewa kwa ajili ya kuwakinga wananchi na magonjwa ya mlipuko ikiwemo kipindupindu,  ambacho kilikuwemo mkoani humo wiki mbili zilizopita, kutibu maji ili yawe salama.

Akipokea misaada hiyo Dk Jesca, alisema kuwa misaada hiyo imekuja wakati muafaka ambapo itasaidia kukabili magonjwa ya mlipuko na magonjwa ya matumbo ambayo hutokea mara kwa mara.

Dk.Lebba alisema kuwa wakati huu wa mvua kumekuwa na changamoto kubwa ya magonjwa ya tumbo, kuhara na kipindupindu yanayotokana na kuchafuliwa kwa maji na uchafu wa aina mbalimbali,  hivyo dawa hizo zitasaidia kutibu maji na kuyafanya kuwa safi na salama kwa matumizi.

Akizungumzia uwepo wa ugonjwa wa kipindupindu alisema kuwa kwa sasa ugonjwa huo umedhibitiwa baada ya kulipuka mji mdogo wa Nguruka wilaya ya Uvinza, ambapo watu sabu walilazwa na baadaye kuruhusiwa na hakuna kifo kilichotokea.

Habari Zifananazo

Back to top button