WATOTOT 427 wenye matatizo ya matundu kwenye moyo, matatizo ya mishipa ya damu na Valve za moyo wamefanyiwa uchunguzi katika kambi ya matibabu ya wiki moja Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo jijini Dar es Salaam.
Kati ya watoto hao 41 walifanyiwa upasuaji kwa njia ya tundu dogo ambao umefanyika kupitia mtambo wa Cathlab na watoto 18 wamefanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo wa kufungua kifua.
Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa kambi hiyo, Mkurugenzi wa Upasuaji wa JKCI, Dk Angela Muhozya, alisema kambi hiyo ilianza Mei 12 hadi 19, ambapo JKCI kwa kushirikiana na madaktari kutoka Mradi wa Little Heart wa Shirika la Muntada Aid kutoka London,Uingereza.
“Hawa ni madaktari ambao wamekuwa wakija katika Taasisi ya moyo kwa miaka saba mpaka sasa na wanakuja kwa ajili ya matibabu ya magonjwa ya moyo kwa watoto na kwa kawaida wakija huwa tunafanya uchunguzi kwa watoto wengi na wengine wanapitiwa huduma za upasuaji,” amesema.
Amesema watoto 18 waliofanyiwa upasuaji wengine wameshatoka chumba cha uangalizi maalum, ambapo wamebakiwa watoto watatu.
“Tunawashukuru sana wenzetu kwa kuendelea kufanya kazi na JKCI kwanza wanatujengea uwezo kila mwaka tunaenda hatua mbele na pia wanatuletea vifaa katika kila walichotuelekeza wakirudi tumepiga hatua zaidi,”amesema.