Wilaya Tanganyika wavuka lengo upandaji miche ya miti

ZAIDI ya miche ya miti milioni 2 imepandwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi na kuifanya Halmashauri hiyo kuvuka lengo la kitaifa linaloitaka kila halmashauri kupanda miti isiyopungua milioni 1.5.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika, Onesmo Buswelu, wakati wakiendelea na upandaji miti, alipowaongoza wakuu wa idara mbalimbali na baadhi ya wananchi kupanda miti katika nyumba za watumishi zilizopo eneo la Kijiji cha Majalila Kata ya Tongwe.
Buswelu amesema jumla ya miti 350, imepandwa eneo la pembezoni mwa barabara ya Polisi kuelekea mtaa wa nyumba za watumishi na kufanya jumla ya miti iliyopandwa katika halmashauri hiyo hadi kufika Januari 30 kuwa 2,014,750.
“Nitoe wito kwa wasimamizi wetu wote, viongozi wote kusimamia miti hii istawi vizuri, tunatamani miti hii usife mti hata mmoja na ili isife lazima itunzwe na ilindwe,” ameagiza.
Pia amewaonya wafugaji kulisha kwenye miche iliyopandwa na mazao ya wakulima pamoja na wananchi wanaong’oa na kuiba miche iliyopandwa kuacha tabia hiyo mara moja.
Naye Meneja wa Wakala wa Huduma za Misitu (TFS), Wilaya ya Tanganyika Saimon Peter amesema upandaji miti ni endelevu katika maeneo mbalimbali ya halmashauri hiyo, licha ya kuwa wameshavuka lengo kwa kuwa miti bado ipo kwenye vitalu na watahakikisha inasambazwa kwenye taasisi mbalimbali ili ipandwe.