MWILI wa mkazi wa Usule ambaye ni dereva wa bajaji, Shaban Mangi (40) umekutwa umefukiwa katika shimo baada ya kudaiwa kuuawa na msaidizi wake kwa tuhuma za wivu wa mapenzi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi mkoani Tabora, Richard Abwao alisema tukio hilo lilitokea Aprili 15, mwaka huu majira ya saa 9:00 alasiri katika Kitongoji na Kijiji cha Utusini, Kata ya Misha, Manispaa ya Tabora mkoani hapa.
Alisema mtuhumiwa ambaye jina lake limehifadhiwa kwa uchunguzi zaidi alimpiga na kitu kizito kichwani na kusababisha kifo chake.
Kamanda Abwao alisema Mangi aligundulika ameuawa kisha kufukiwa kwenye shimo na mtuhumiwa huyo huku chanzo kikidaiwa kuwa ni wivu wa mapenzi.
Alisema mtuhumiwa alishirikiana na watu wengine ambao Jeshi la Polisi linaendelea kuwasaka.
Kamanda Abwao alisema mtuhumiwa alikuwa akimtuhumu dereva wake kuwa na mahusiano ya kimapenzi na mpenzi wake.
Mwili wa dereva huyo umehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora, Kitete kwa ajili ya uchunguzi zaidi na mtuhumiwa amekamatwa na atafikishwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika.