WIZARA ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na Uongozi wa Wilaya ya Kilwa imejipanga kuboresha urithi wa kihistoria na malikale ndani ya wilaya hiyo.
Akizungumza leo Mei 11, 2023 kwenye kikao kazi cha kupokea taarifa ya namna mpango jumuishi wa matumizi ya maeneo ya Kilwa Kisiwani na Songo Mnara utakavyo tekelezwa, Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Christopher Ngubiagai amesema ili kuendeleza urithi wa nchi ni lazima maliasili na malikale zitunzwe.
Akisisitiza juu ya umuhimu wa kutunza urithi mbalimbali za nchi, aliwaasa wananchi kuunga mkono juhudi za serikali katika uhifadhi endelevu wa maeneo ya malikale yaliyo kwenye maeneo yao.
“Wakati mwingine historia huwa inahukumu, usipofanya mambo mazuri kwa wakati fulani baadae historia inakuja kukuhukumu kwamba uliyoyafanya wakati wa uongozi wako hayakuwa sahihi…tukiweka mambo vizuri, tukitumia vizuri maeneo haya yatatusaidia baadae kuleta mapato na mchango wa taifa,” Alisema Ngubiagai.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa idara ya malikale nchini Dk Christowaja Ntandu amesema kuwa ni mpango wa wizara kupitia idara anayoiongoza ni kuyaendeleza maeneo mbalimbali ya malikale nchini na kuyafanya kuwa chachu ya maendeleo ya uchumi wa Taifa na wananchi kwa ujumla.
“kilwa inaweza ikawa ndo mfano tukimaliza huu mpango, naweza nikasema baada ya mikindani Kilwa sasa nadhani ndo inaenda kuvunja rekodi,” alisema Dk Ntandu