Wizara kusimamia malengo ya Regrow

WIZARA  ya Maliasili na Utalii inaendelea kuimarisha mikakati yake ya usimamizi wa Mradi wa Kuboresha Usimamizi wa Maliasili na Kukuza Utalii Kusini mwa Tanzania (REGROW) kupitia mafunzo maalum ya kuandaa na kusimamia mpango na rejesta ya viashiria  hatarishi katika kufikia malengo ya mradi.

Akifungua mafunzo  mkoani Morogoro, Mkurugenzi wa Sera na Mipango, Wizara ya  Maliasili na Utalii,  Abdallah Mvungi amesema wizara imeona umuhimu wa kutoa mafunzo ya usimamizi na kushughulikia  vihatarishi   ili kuwaongezea uwezo wataalam wake wawe na  uwelewa mpana katika kupambana na viashiria hivyo kwenye mradi wa REGROW.

“Mafunzo haya ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuhakikisha mradi huu unafikia malengo kwa maslahi mapana ya Taifa na mwananchi mmoja mmoja, hivyo niwatake washiriki wote mzingatie mafunzo haya ili mkawe mabalozi wazuri katika utekelezaji wa mpango huu”. amesema  Mvungi

Aidha, Mvungi amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa jitihada mbalimbali kubwa anazochukua katika kuboresha usimamizi wa maliasili na kukuza utalii nchini hususan kusini mwa Tanzania, kupitia mradi huo.

Akimkaribisha mgeni rasmi, Naibu Msimamizi wa Mradi wa REGROW  Blanka Tengia ameeleza kuwa  mafunzo hayo yanayoendeshwa na wakufunzi kutoka Idara ya Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Serikali (IAGD), Wizara ya Fedha,  yanatolewa kwa nadharia na vitendo hali ambayo itawafanya washiriki kuweza kupata ujuzi wa kuandaa na kusimamia mpango huo na kutekeleza rejesta ya vihatarishi hivyo kwa ufanisi.

Tengia   ameongeza kuwa mradi huo wenye lengo la kuboresha usimamizi wa maliasili na kukuza utalii Kusini mwa Tanzania unatekelezwa katika hifadhi za Taifa za kipaumbele za Ruaha, Udzungwa, Mikumi, Nyerere  na Hifadhi ya Msitu wa Asili Kilombero kwa mkopo wa masharti nafuu kutoka Benki ya Dunia.

Habari Zifananazo

Back to top button