Wizara kutathmini madaktari bingwa hospitali za mikoa

WIZARA ya Afya itafanya tathmini kwenye hospitali za rufani za mikoa kutokana na kuwa na idadi kubwa ya madaktari bingwa kuliko maeneo ya pembezoni.

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alisema hayo wakati akitoa ufafanuzi wa maswali mbalimbali ya wabunge jana bungeni waliohoji upungufu wa madaktari hao kwenye maeneo yao.

Alisema Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, (Jenista Mhagama) ameshatoa kibali kufanyika tathmini hiyo.

Alisema ikibainika wamezidi, watahamishwa na kupelekwa maeneo yenye shida wakati wakisubiriwa wanaosomeshwa ambapo aliahidi ndani ya miaka miwili itakuwa ni historia kutokana na Mpango wa Rais Samia Suluhu Hassan.

Alisema serikali ina mpango maalumu wa kusomesha madaktari bingwa na madaktari bingwa bobezi ambapo kwa mwaka huu wa fedha 2022/23, watasomeshwa 139 na kati yao, 136 watasomeshwa nje ya nchi na waliobaki nchini.

“Wanasomeshwa kwa seti yaani daktari bingwa, mtaalamu wa usingizi, mtaalamu wa mionzi. Tuna madaktari bingwa 457 wanasomeshwa kwa seti moja moja kwa sasa,” alisema.

Ummy alitoa maelezo hayo kutokana na swali la msingi, la Mbunge wa Viti Maalumu, Tecla Ungele (CCM), aliyehoji lini serikali itaona umuhimu wa kupeleka madaktari bingwa wa magonjwa ya ndani na mifupa katika Hospitali ya Rufani Mkoa wa Lindi.

Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel, alisema hadi sasa hospitali hiyo ina madaktari bingwa watano ambao ni daktari bingwa wa upasuaji, daktari bingwa wa mionzi na daktari bingwa wa dawa za usingizi na wawili ambao ni madaktari bingwa wa afya ya uzazi na mtoto wawili.

“Katika kuongeza idadi ya madaktari bingwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Lindi, wizara imepeleka kusoma jumla ya madaktari saba,” alisema.

Kuhusu daktari bingwa wa magonjwa ya ndani, alisema serikali inakamilisha taratibu za uhamisho ili kumpeleka hospitali ya Lindi.

Habari Zifananazo

Back to top button