WIZARA ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara imelieleza Bunge kuwa hadi Machi mwaka huu nchi ina viwanda 14 vya saruji vinavyokidhi mahitaji na kubaki na ziada.
Waziri wa wizara hiyo, Dk Ashatu Kijaji amesema kati ya hivyo 14 viwanda vikubwa viko saba na vilivyobaki vinazalisha saruji kutokana na clinker iliyozalishwa na viwanda hivyo saba.
Dk Kijaji alisema takwimu za uzalishaji wa saruji kwa mwaka jana zinaonesha viwanda hivyo vinazalisha tani 10,850,000.
Aliwaeleza wabunge kuwa mahitaji ya ndani ya nchi ni tani 7,100,000 kwa mwaka hivyo kuna ziada ya tani 3,750,000 inayouzwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Rwanda, Uganda, Malawi, Zambia na Msumbiji.
Dk Kijaji alisema hayo bungeni Dodoma wakati anawasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2023/24.
Kuhusu viwanda vya kuzalisha bidhaa za chuma, Dk Kijaji alisema katika kipindi cha mwaka 2020 hadi mwaka jana matumizi ya bidhaa za chuma nchini yameongezeka kutoka tani 226,000 hadi kufikia tani 1,000,000 kwa mwaka sawa na ongezeko la asilimia 303.54.
Alisema hadi Machi mwaka huu Tanzania ilikuwa na viwanda 25 vya kuzalisha chuma na bidhaa za chuma.
Dk Kijaji alisema kuna viwanda 16 vya kuzalisha vyenye uwezo uliosimikwa wa kuzalisha tani 1,082,700 kwa mwaka na uzalishaji halisi ni tani 750,000 kwa mwaka sawa na asilimia 69 ya uwezo uliosimikwa.
“Mahitaji ya nondo nchini kwa mwaka ni tani 550,336. Hivyo uzalishaji huo wa ndani hutosheleza mahitaji yote ya ndani na ziada kiasi cha tani 199,664 huuzwa nje ya nchi,” alisema.
Kuhusu viwanda vya mabati, Dk Kijaji alisema hadi kufikia Machi mwaka huu Tanzania ina viwanda viwili vikubwa vinavyozalisha mabati kuanzia hatua ya awali ambavyo ni ALAF na MMI Steel vyenye uwezo uliosimikwa wa kuzalisha jumla ya tani 158,000 kwa mwaka na uzalishaji halisi ni tani 58,189 kwa mwaka sawa na asilimia 37 ya uwezo uliosimikwa.
Alisema viwanda vinavyozalisha bidhaa za chuma vimeajiri wafanyakazi 23,588 wakiwamo 3,588 wa ajira ya moja kwa moja na 20,000 ni ajira za muda.
Aidha, Dk Kijaji alisema hadi Machi mwaka huu nchi ina viwanda 17 vya mbolea vikiwamo viwili vikubwa ambavyo ni Minjingu na Intracom Fertilizer Limited, kimoja ni kiwanda cha kati na viwanda vidogo 14.
Alisema kiwanda cha Intracom Fertilizer Limited kilichopo Dodoma kinatarajia kuwekeza mtaji wenye thamani ya dola za Marekani milioni 180 na kitakuwa na uwezo kuzalisha tani 200,000 kwa mwaka na kutoa ajira za kudumu 3,000 na ajira zisizo za kudumu zaidi ya 8,000.
Kwa upande wa kiwanda cha Minjingu kimewekeza Sh bilioni 50 na kina uwezo wa kuzalisha tani 120,000 za mbolea kwa mwaka.