Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inafanya mapitio ya sheria ya elimu ili kuhakikisha adhabu kali zinatolewa kwa wanaoshiriki kufanya vitendo vya udanganyifu katika mitihani ya kitaifa.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam, Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Prof Adolf Mkenda, amesema wizara hiyo inaongea na mamlaka husika ili wanaovujisha na kufanya vitendo vya udanganyifu katika mitihani wasiishie kufukuzwa kazi tu bali wachukuliwe hatua za kisheria kwa kuwa vitendo hivyo ni vya jinai.
Waziri huyo alisisitiza kwa kusema imebainika kuwa baadhi ya watumishi wa umma wasio waaminifu hushiriki katika vitendo hivyo huku akisema haina utofauti na uhujumu uchumi.
“kuna hata watumishi wa umma ambao wanashiriki katika udanganyifu, nisisitize kwamba unapotaka kuua taifa basi chezea elimu, nasi hatutakubali kuona taifa linaharibiwa na watu wachache wasio waaminifu,” amesisitiza waziri.
Aidha alisema moja ya madhara ya udanganyifu katika mitihani ni kuzalisha wataalamu wasiokuwa na viwango kutokana na kumwezesha mtu ambaye hakustahili kuendelea na masomo kusonga mbele.
Kwa kuongezea alisema, Baraza la Mitihani la Tanzania limeongeza Mikakati ya kupambana na watu ambao wanafanya udanganyifu kwenye mitihani na kubaini shule mbalimbali ambazo wasimamizi pamoja na walimu wameshirikiana kwa namna moja au nyingine kufanya udanganyifu huo.
Desemba 1, 2022 Baraza la mitihani la Taifa lilitangaza matokeo ya darasa la saba ambapo shule 24 zilifungiwa kuwa vituo vya mitihani ya Taifa baada ya kuthibitika kupanga kufanya udanganyifu katika mitihani ya kumaliza elimu ya msingi.