Wizara ya Elimu, TET, GMOE, GERIS kuimarisha Tehama

WIZARA ya Elimu, Sayansi na Teknolojia (WyEST) kupitia Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) na Ofisi ya Elimu ya Gwangju Metropolitan (GMOE) kupitia Global Education and Research Information Service (GERIS) zimesaini hati ya makubalino ya miaka minne katika mradi wa kuimarisha matumizi ya TEHAMA nchini.

Hati hizo zimesaini leo Novemba 7, 2023 jijini Dar es Salaam kwa lengo la kuimarisha matumizi ya TEHAMA katika ufundishaji na ujifunzaji.

Akizungumza Mkurugenzi Mtendaji wa TET, Dk Anneth Komba amesema makubaliano matatu yaliyofikiwa ni ofisi ya Elimu ya Gwangju itaipatia Taasisi ya Elimu kila mwaka kompyuta na vifaa vingine vya TEHAMA na TET itawajibika kulipia gharama za kuvikomboa vifaa hivyo bandarini pamoja na na gharama ya kuvisafirisha katika shule husika.

Pia, Gwangju itaandaa na kuwaalika kuhudhuria mafunzo nchini Korea wataaluma, walimu na watumishi wengine wa umma kutoka wizara ya Elimu juu ya matumizi ya TEHAMA katika ufundishaji na ujifunzaji pamoja na mambo mengine ya Kielimu. Mafunzo haya yatafadhiliwa na Ofisi ya Elimu ya Gwangju ikiwemo tiketi ya kwenda na kurudi nchini Korea, chakula na malazi nchini Korea.

“Ofisi ya Elimu ya Gwangju itatoa wataalamu kuja Tanzania kutoa mafunzo na itabeba gharama zote za mafunzo hayo ikiwemo gharama za safari ya kuja na kurudi na malazi,”amesema.

Naye, Kamishna wa elimu wa Gwangju, Lee Wang Do akizungumza amesema Tanzania ina fursa na rasilimali nyingi ikiwemo Mlima Kilimanjaro na mbuga za Wanyama kama Ngorongoro, Serengeti na nyingine, ametembelea shule ya Tegeta A na kwamba mazingira waliyoyakuta ni kama shule za Korea Kusini miaka 50 iliyopita.

“Korea pia zilikuwa hivi hivi lakini ukiwa na nia na hari, mkawa na ndoto za kufikia malengo basi mtafanikiwa, hata Korea iliwahi kusaidiwa na nchi zilizoendelea, lakini wananchi tuliamua kufanya kazi kwa bidii ndio Korea mnayoiona leo, naamini kama Tanzania inataka kupiga hatua basi mkichukua Korea kama mfano ‘role model’ katika TEHAMA tutashukuru sana.”Amesema.

Habari Zifananazo

Back to top button