Wizara ya Viwanda yaomba kuidhinishwa Sh bil 110.9

DODOMA: WIZARA ya Viwanda na Biashara imeliomba Bunge kuidhinisha bajeti ya Sh bilioni 110.9 kwa mwaka wa fedha 2024/2025 ili kutekeleza vipaumbele vikuu sita.

Hayo yameelezwa leo na Waziri wa viwanda na Biashara, Ashatu Kijaji wakati akisoma makadirio ya mapato na matumizi ya wizara kwa mwaka wa fedha 2024/2025, leo Mei 21, 2024 bungeni jijini Dodoma.

Isome pia: https://habarileo.co.tz/dk-ashatu-ataka-kasi-ya-utendaji-wizara-ya-viwanda/

Advertisement

Dk Kijaji ametaja vipaumbele hivyo kuwa ni kuendelea na utekelezaji wa miradi ya kielelezo na kimkakati, kuimarisha uwezo wa uzalishaji viwandani na utoaji huduma kwa kuimarisha miundombinu na mazingira wezeshi.

Pia, amesema vipaumbele vingine ni kuboresha mazingira ya uwekezaji viwandani na ufanyaji biashara, kuchochea maendeleo ya watu kwa kuboresha miradi na programu katika sekta za kiuchumi na kijamii inayohusisha elimu na mafunzo ya ujuzi.

Ametaja kipaumbele kingine kuwa ni kufanya intelijensia ya masoko ya bidhaa na huduma zinazozalishwa nchini kwenye masoko ya kimkakati ya kimataifa ili kuchochea ukuaji wa sekta binafsi nchini.