Wahalifu wasakwa nyumba kwa nyumba
GEITA; JESHI la Polisi mkoani Geita limetangaza kuanza oparesheni ya nyumba kwa nyumba inayolenga kuwasaka, kuwafichua na kuwakamata watu wote wanaojihusisha na shughuli haramu na uhalifu mkoani humo.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Geita, Safia Jongo ametoa kauli hiyo katika mazungumzo na waandishi wa habari juu ya mikakati ya kuimarisha ulinzi na usalama.
Amesema oparesheni ya nyumba kwa nyumba imeanza mapema mwezi Oktoba 2023 na itaenda mpaka mwishoni wa mwaka huu, ili kudhibiti aina yeyote ya matukio ya uhalifu ya mwisho wa mwaka.
“Kama mnavyojua mwisho wa mwaka kila mtu anatafuta hela ya ada, anatafuta hela ya sikukuu, na ndiyo maana uvunjaji wa sheria unaongezeka kuanzia barabarani mpaka huko mitaani.
“Hii oparesheni sisi tumeianza mapema, kuhakikisha kwamba watu wa Geita, sikukuu za Krismasi na mwaka mpya kwa wale wanaotafuta kipato kwa halali basi watasherehekea vizuri.
“Lakini kwa wale wanaotegemea wawaibie watu ndiyo waishi, basi waanze kutafuta shughuli za kufanya kwa sababu mwanya huo haupo, tutakusaka popote ulipo kuhakikisha wananchi wanakuwa salama,” amesema.
Kamanda Jongo amewaelekeza watendaji wa mitaa, vijiji na kata kulisaidia jeshi la polisi kufanikisha oparesheni hiyo kwa kuanzisha vikundi vya ulinzi shirikishi, ili kuwafichua wahalifu kwenye maeneo yao.