Wizara yahadharisha matamasha utalii wa ndani

WIZARA ya Maliasili na Utalii imeutahadharisha umma uwe makini na matamasha ya kutangaza utalii wa ndani

Taarifa ya kitengo cha mawasiliano serikalini katika wizara hiyo imeeleza kuwa haihusiki kwa namna yoyote katika maandalizi au uchangishaji wa fedha kutoka kwa wananchi na wadau ili kutangaza utalii wa ndani kupitia matamasha yaliyojificha chini ya kivuli cha filamu ya The Royal Tour.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo kwa umma jana, filamu hiyo imechochea mwamko wa shughuli na matukio ya kuhamasisha utalii wa ndani kama vile chakula cha hisani na matamasha ya muziki ambayo yamekuwa yakihusisha uchangishaji wa fedha za kiingilio na wakati mwingine kutoa matangazo ya ushiriki wa viongozi wakuu wa serikali akiwemo Rais Samia Suluhu Hassan ili kuwavutia wananchi.

Ilieleza kuwa kazi iliyofanywa na Rais Samia kuvitangaza vivutio vya Utalii vya Tanzania na fursa za uwekezaji kupitia filamu ya Tanzania The Royal Tour imekua na matokeo chanya kutokana mwitikio wa ujio wa watalii na wawekezaji wanaokuja kuwekeza nchini Tanzania.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa sekta ya utalii nchini imepata mafanikio kutokana na juhudi zilizofanywa na serikali kwa kushirikiana na wadau za kusimamia utekelezaji wa mikakati ya kukuza vivutio vya utalii zikiwemo hifadhi za wanyamapori, maporomoko ya maji, milima, misitu ya mazingira asilia, utamaduni, fukwe na malikale.

“Wizara ya Maliasili na Utalii imepewa dhamana ya kusimamia uhifadhi wa maliasili, malikale na maendeleo ya utalii hapa nchini. Wizara inatekeleza majukumu haya kwa kuzingatia sera, sheria, kanuni, mipango ya maendeleo na maelekezo mbalimbali ya serikali”ilieleza taarifa hiyo.

Hivi karibuni Mkurugenzi wa Takwimu za Uchumi kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Daniel Masolwa alisema idadi kubwa ya watalii walioingia nchini Julai mwaka huu imeongezeka kutoka 81,307 wa Julai mwaka jana hadi 166,736 wa mwaka huu sawa na ongezeko la asilimia 105.1.

Rais Samia amesema filamu hiyo itaongeza watalii nchini na mapato yanayotokana na sekta ya utalii.

Alisema hayo alipozungumza na wananchi alipowasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) akitoka Marekani.

Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi alisema filamu ya Royal Tour ni fursa ya kuitangaza Jamhuri ya Muungano katika sekta ya utalii na vivutio vyake kuingia katika soko la utalii duniani.

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button