Wizara yajizatiti utatuzi migogoro ya ardhi

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Ridhiwani Kikwete

WIZARA ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kushirikiana na wizara nyingine za kisekta zitaendelea kudhibiti na kushughulikia migogoro na kuitafutia ufumbuzi iliyopo ili kuimarisha ustawi wa jamii baina ya wakulima na wafugaji.

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Ridhiwani Kikwete alisema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Mlimba, Godwin Kunambi (CCM) aliyetaka kufahamu ni lini serikali itatatua migogoro ya wakulima na wafugaji katika Jimbo la Mlimba.

Ridhiwani alijibu: “Serikali inatambua uwepo wa changamoto mbalimbali zinazosababisha migogoro ya matumizi ya ardhi ikiwemo hiyo ya wakulima na wafugaji.”

Advertisement

Serikali imechukua hatua mbalimbali kuhakikisha migogoro ya matumizi ya ardhi katika Mkoa wa Morogoro hususani Wilaya ya Kilombero inatatuliwa.

Miongoni mwa hatua zilizochukuliwa ni pamoja na kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi na kumilikisha ardhi kupitia Mradi wa Kuwezesha Umilikishaji wa Ardhi (LTSP) ambapo jumla ya vijiji 58 viliandaliwa mipango ya matumizi ya ardhi na hati za hakimiliki za kimila 150,006 zilisajiliwa.

Kati ya vijiji hivyo 58, vijiji 32 viko katika Halmashauri ya Mlimba ambapo katika halmashauri hiyo jumla ya hati za hakimiliki za kimila 41,797 zimesajiliwa na 30,699 zimechukuliwa na wananchi.

Hatua iliyochukuliwa na serikali ni kudhibiti na kuimarisha utatuzi wa migogoro kwa kutoa elimu kupitia mikutano ya wananchi kuhusu mipango ya matumizi ya ardhi iliyowekwa pamoja, kutungwa kwa kanuni za usimamizi wa matumizi ya ardhi na kuhimiza matumizi ya ardhi yenye tija.

Alisema wizara kwa kushirikiana na wizara nyingine za kisekta zitaendelea kudhibiti na kushughulikia migogoro na kuitafutia ufumbuzi iliyopo ili kuimarisha ustawi wa jamii baina ya wakulima na wafugaji.