Wizara yaongeza siku malalamiko ya ardhi

Wizara yaongeza siku malalamiko ya ardhi

WIZARA ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, imeongeza siku tatu za kusikiliza changamoto mbalimbali za ardhi  katika jiji la Dodoma.

Akizungumza na waandishi wa habari  jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dk Allan Kijazi, amesema hatua hiyo inakuja mara baada ya wananchi kuendelea kujitokeza kupeleka kero.

“Malalamiko hayo mengine yalikuwa yanahitaji ufafanuzi wa kina na kuna wananchi walikuwa wanalalamika kuwa hawajapata nafasi ya kusikilizwa,  hivyo tumeona ni bora kuongeza siku,”amebainisha na kueleza kuwa awali ilikuwa siku mbili Septemba 29 na 30 mwaka huu.

Advertisement

Hata hivyo amesema sasa wataendelea na jukumu hilo, Oktoba 17, 2022 kwa wakazi wa maeneo ya  Kizota, Nkuhungu na Nara  kuanzia saa mbili asubuhi  hadi sasa 10 jioni katika ofisi ya Kata ya Kizota.

Ameeleza kuwa wananchi wa maeneo ya Mnadani na Miyuji malalamiko yao yatasikilizwa Oktoba 18, 2022 kuanzia asaa mbili asubuhi hadi saa 10 jioni katika ofisi za kata Miyuji.

“Siku ya tatu ni wananchi wa maeneo ya Mtumba, Chahwa na Ibara tunawapa nafasi ya kuwasilisha  malalamiko yao Oktoba 19, 2022 katika ofisi ya kata ya Chahwa,”ameeleza Dk kijazi.

Amesema kuna haja ya watalamu wao kabla ya kutoa mrejesho  kwa baadhi ya malalamiko  kutoa elimu, kufanya ukaguzi.