NAIBU Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Selestine Kakele ameipongeza Kampuni ya Magazeti ya Serikali Tanzania (TSN) kwa kuendelea kutoa huduma zenye viwango na kwa weledi.
Kakele alisema hayo alipotembelea banda la TSN katika Maonesho ya 47 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF) yanayoendelea katika Viwanja vya Sabasaba.
Kakele jana alitembelea banda hilo na kupewa maelezo ya huduma zinazotolewa na TSN ambao ni wachapishaji wa magazeti ya HabariLEO, HabariLEO Jumapili, Daily News, Sunday News na magazeti ya mtandao.
Baada ya kupata maelezo, alisema TSN ni moja ya taasisi za serikali zinazotoa huduma ya habari na imekuwa ikifanya kazi yake kwa weledi na kuitaka iendelee kutekeleza majukumu yake hayo.
“Niwapongeze kwa kufanya kazi kwa weledi, mnafanya kazi nzuri. Naamini mkikamilisha ujenzi wa mtambo mpya wa uchapaji, matumaini ni kuwa huduma zitaendelea kuboreka zaidi. Serikali itaendelea kuwasaidia katika kutimiza majukumu yenu,” alisema.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TSN, Tuma Abdallah alihimiza washiriki wa maonesho hayo kutembelea banda la TSN kujionea huduma inayotolewa ikiwa ni pamoja na huduma za habari mtandao, ushauri, majarida ya elimu ambayo yamekuwa msaada kwa wanafunzi kupata maarifa zaidi.
“Moja ya bidhaa tunazotoa, ni majarida ya elimu ambayo tunasaidia sekta ya elimu na tunatoa bure ndani ya magazeti yetu mara moja kwa wiki.
“Tunayaandaa kwa kushirikiana na walimu mbalimbali na yanakwenda kulingana na wakati na mihula ili kuwaandaa wanafunzi na imekuwa nyenzo moja ya kuboresha maendeleo ya kielimu ya wanafunzi,” alisema Tuma.
Alisema TSN inaenda na mabadiliko ya teknolojia kwa kuanzisha huduma ya magazeti mtandao ambayo yanatoa fursa kwa wasomaji kulisoma gazeti lote kupitia mtandao na hiyo ni fursa ya kuliuza popote duniani kwa ubora ule ule.