TAASISI tatu zilizoko chini ya Wizara ya Kilimo, zimeridhishwa na uwekezaji unaofanywa na Kampuni ya Global Agency katika kuhakikisha inazalisha mbegu bora za mahindi, ngano na soya.
Hatua ya kampuni hiyo itasaidia kuendana na lengo la serikali kuhakikisha nchi inajitoshekeza katika mazao ya mbegu na kupunguza gharama za kuagiza mbegu za mazao nje ya nchi.
Taasisi hizo ni ya utafiti wa mazao (TARI), Wakala wa Uzalishaji Mbengu za Mazao (ASA) na Wadhibithi wa Ubora wa Mbengu (TOSIC), ambapo waliambatana na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Mazao Wizara ya Kilimo, walitembelea shamba la mwekezaji huyo anayezalisha mbegu za mazao mbalimbali Kijiji cha Buchurago, Kata ya Bugorora wilayani Missenyi.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Mazao, Nyasebwa, alisema timu hiyo ilifika katika shamba la mwekezaji huyo, ikiwa ni maagizo ya Waziri wa Kilimo Husseni Bashe.
Amesema lengo la ziara yao ni kuhakikisha kama mbegu zinazozalishwa na ni bora, ni kwa jinsi gani serikali inaweza kumuunga mkono mwekezaji huyo katika jitihada zake za kupunguza uhaba wa mbegu bora nchini.
Alisema timu hiyo imejiridhisha kwamba mbegu zinazozalishwa ni bora na zinakidhi vigezo vyote vinavyohitajika.
Mbegu zilizokaguliwa za mahindi aina mbalimbali, ngano aina ya kalyege na mbegu ya soya.
“Sio mara ya kwanza kufika katika shamba hili, mwaka 2020 tulifika kama wizara na timu hii, tulifanya ukaguzi na bado kulikuwa na changamoto nyingi, lakini kwa sasa tunafurahishwa na mwekezaji, ambavyo ametumia changamoto za awali na kufanya shamba lake kuwa bora zaidi.
“Ni wakati sasa wa serikali kumuunga mkono na kumpa nguvu ya kuendelea kuzalisha zaidi,”alisema Chimagu.
Sophia Kashenge, ambaye ni Mtendaji Mkuu ASA, alisema serikali imeongeza bajeti kwa wazalishaji binafsi, ambao wamejitolea kuzalisha mbegu bora, hivyo Global Agency atanufaika na bajeti hiyo, ambapo amefurahishwa pia na mitambo ya umwagiliaji inayotumika katika shamba hilo.
Furaha Mroso, ambaye ni Meneja Mtafiti wa mazao kutoka TARI, alisema baada ya ukaguzi TARI wako tayari kutoa mbegu zinazokubalika, ambazo zinaweza kuwasaidia wakulima kuongeza kipato chao kwa kupanda mbegu hizo.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Global Agency, Fidelis Bashasha, alisema amefurahishwa na utendaji kazi wa Serikali ya Awamu ya Sita, juu ya kutekeleza ahadi na kufatilia juhudi za wawezaji, wenye ndoto ya kulisaidia taifa kupunguza gharama za kuagiza mbegu za chakula kutoka nje ya nchi.
Alisema shamba lake lina hekari 21 na anajaribu kuleta mabadiliko mkoani Kagera, katika kuanzisha kilimo cha mazao ambayo hayajazoeleka, hivyo kuiomba serikali imuunge mkono aweze kuzalisha mbegu za mazao mbalimbali.