Wizara yasitisha uchimbaji madini Kwandege

WIZARA  ya Madini kupitia Ofiisa Mfawidhi wa Madini Mkoa wa Tanga, Zabibu Napacho imesitisha shughuli za uchimbaji dhahabu katika kijiji cha Kwandege kata ya Lang’ata wilayani Handeni.

Hatua hiyo imetokana na mgogoro uliopo baina ya mmiliki wa mgodi huo, Godfrey Bitesigirwe na wenye maduara na kwani kunaweza kuhatarisha usalama na amani katika eneo hilo.

Napacho alisitisha shughuli za uchimbaji katika taarifa yake ya Juni 6 mwaka huu katika mgodi wa dhahabu wenye lesseni ya uchimbaji mdogo na uchenjuaji madini –PML 0330-0337TNG-Kwandege na kusema kuwa agizo hilo ni maagizo ya Mkuu wa Wilaya ya HandeniAlbert Msando.

Advertisement

Alisema agizo hilo ni kufuatia kikao cha pamoja kati ya Mkuu wa Wilaya pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya hiyo ,viongozi wa chama na serikali na mmiliki wa mgodi huo katika kikao kilichofanyika juni 6 mwaka huu katika shule ya msingi Kilimazinga.

Ofisa madini huyo alisema kuwa agizo hilo limetolewa kutokana na mgogoro uliopo kati ya Bitesigirwe na wenye lesseni zingine katika eneo hilo lengo ni kutoa nafasi ya kufanyika kwa hatua mbalimbali zitakazopelekea kutatuliwa kwa mgogoro huo kwa utulivu na amani.

‘’Aidha Mkuu wa Wilaya ya Handeni ameagiza kusitishwa kwa shughuli za uchimbaji na uchenjuaji wa Madini kwenye lesseni zako PML0330-0337TNG zilizopo eneo la  Kwandege Kijiji cha Kilimamzinga’’alisema nakala ya Afisa Madini.

Hata hivyo Bitesigirwe alionyesha kutokukubaliana na agizo hilo na kutoa sababu nane za kupinga agizo hilo ikiwa ni pamoja na kuzuia kwake kuendesha shughuli za uchimbaji zinatoa mwanya kwa uchimbaji usio rasmi kuendelea katika mgodi wake kwani hatua hiyo haina tija kwa pande tatu yenye mwenyewe, Serikali Kuu ,Halmashauri na Tume ya Madini kwani dhahabu inayopatikana inatoroshwa na kuuzwa kusikojulikana na kuitia hasara serikali.

Bitesigirwe alisema kuwa alinunuwa mashine kubwa na za kisasa za uchimbaji na uchenjuaji zenye gharama kubwa na kuaminika katika benki ya NBC na kukopeshwa mamilioni ya pesa hivyo hutakiwa kufanya marejesho kila mwezi lakini kutokana na hali hiyo huenda akashindwa kufanya hivyo na wachimbaji wadogo wadogo kushindwa kuaminika katika benki.

Alisema yeye hana mgogoro wowote na wachimbaji wadogo wadogo wa dhahabu katika kijiji cha kwandege bali kuna madalali wa dhahabu{Broker’s} wanaosafiri kwenye migodi ya dhahabu Nchi ndio wanaochochea mgogoro huo na kutoa taarifa za uongo kwa viongozi wa juu wa serikali hatua ambayo haileti afya kwa wakazi wa Handeni.

Mwekezaji huyo mzawa alisema yeye anamiliki leseni nane za dhahabu katika eneo la Kijiji cha Kwandege alizopewa mwaka 2019 kwa kufuata taratibu zote za Tume ya Madini na alianza uchimbaji mwaka 2020 na katika muda wote hakuwahi kuwa na ugomvi na Kijiji,wachimbaji wengine wala viongozi wa chama na serikali ngazi zote anashindwa kujua ni sababu zipi zimepelekea yeye kusitishiwa shughuli za uchimbaji kwani sababu zilizoelezwa yeye anaziona hazina mashiko.

Alisema kuwa toka ameanza uchimbaji amekuwa na ushirikiano mkubwa na wamiliki wengine wa lesseni nne na pia amekuwa akitumia mamilioni ya fedha kwa huduma za jamii kama vile ujenzi wa zahanati,utengenezaji wa madawati na milango,ametoa msaada wa nondo na simenti na upanuzi na ukarabati wa barabara  ya kutoka Kilimamzinga hadi Kijijini kwandege.

Akizungumzioa tukio hilo,Mkuu wa Wilaya ya Handeni,Albert Msando alikiri kumwagiza Afisa Madini kusitisha shughuli za uchimbaji dhahabu katika lesseni hiyo na kusema kuwa hiyo ni kutokana na wahusika kupewa muda mwingi kukaa chini na kutafuta suluhisho lakini ilishindikana.

Msando alisema yeye kama Mwenyekiti wa Ulinzi wa Usalama wa Wilaya ya Handeni hataki kuona mgogoro wowote ndani ya Wilaya hiyo hususani katika machimbo ya dhahabu kwani amani iikitoweka viongozi wa juu watamuuliza yeye sio mtu mwingine yoyote.

Alisema na kuwataka wachimbaji wa dhahabu Handeni wenye lesseni na wasiokuwa na lesseni kufuata taratibu pindi kunapotokea mgogoro katika migodi wanayochimba ikiwa ni pamoja na kuwashirikisha viongozi wa serikali ngazi ya kijiji, kata, wilaya na mkoa.

1 comments

Comments are closed.