WIZARA tatu ikiwamo ya Kilimo, Afya na Maji zinatarajiwa kuwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka wa fedha 2023/24 wiki hii katika mkutano wa 11 wa Bunge.
Wiki iliyopita Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara ziliwasilisha bajeti zao bungeni, zikajadiliwa na kupitishiwa.
Leo, Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe anatarajiwa kuwasilisha bajeti ya wizara hiyo ambayo itajadiliwa kwa siku mbili.
Katika bajeti iliyowasilishwa mwaka jana, Bashe alitaja vipaumbele 10 vya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2022/23 kuwezesha ukuaji wa sekta hiyo hadi asilimia 10 ifikapo mwaka 2030.
Miongoni mwa vipaumbele katika bajeti hiyo ni kuimarisha utafiti, kutoa ruzuku ya mbegu za alizeti, ngano na miche ya chikichiki na kuimarisha upatikanaji wa pembejeo za kilimo.
Bashe alisema ili kufikia lengo la sekta hiyo ya kilimo kukua kwa asilimia 10, bajeti hiyo ilijiwekea malengo ambayo ni kujitosheleza kwa mahitaji ya chakula ndani na nje ya nchi na kuuza nje ya nchi.
Malengo mengine ni kuongeza eneo la kilimo cha umwagiliaji, kuongeza ajira za kilimo kwa wanawake na vijana zitakazofikia milioni moja ifikapo mwaka 2025 na kuhakikisha upatikanaji wa malighafi kwenye viwanda unafikia asilimia 100 ifkapo mwaka 2030.
Baada ya bajeti ya Kilimo, keshokutwa Mei 10, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso anatarajiwa kuwasilisha makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2023/34.
Maeneo mengine yanayotarajiwa kuibuka katika mjadala wa bajeti hiyo ni miradi ya maji, mradi wa maji wa miji 28 uliozua mjadala bajeti iliyopita, upotevu wa maji, ankara za maji, mabadiliko ya tabianchi yanayosababisha ukame na maji kupungua na mita za maji za kulipia kabla ya matumizi.
Mei 12 mwaka huu Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu anatarajiwa kuwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2023/24.
Bajeti hiyo pia inatarajiwa kuibua mjadala katika maeneo ya vifaa vya tiba, ujenzi wa vituo vya afya na zahanati, upatikanaji wa dawa kwa wakati, magonjwa ya mlipuko na uhaba wa watumishi katika zahanati, vituo vya afya na hospitali.
Katika bajeti ya mwaka wa fedha 2022/23 serikali ililieleza Bunge kuwa ilitenga Sh trilioni 1.1 kwa ajili ya kutekeleza pia vipaumbele 13 ili kuboresha huduma za afya.
Kwa mujibu wa ratiba ya Bunge, Bajeti Kuu ya serikali inatarajiwa kusomwa Juni 15 mwaka huu saa 10:00 jioni na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba.