WMO yatabiri ongezeko la joto duniani
GESI chafuzi za viwandani na matukio ya kimaumbile ya El-Nino imetajwa kuwa ni sababu itakayopelekea kuongezeka kwa kiwango cha juu zaidi cha joto duniani kwa miaka mitano ijayo. Shirika la Utabiri wa Hali ya Hewa Duniani WMO limeleeza.
Taarifa ya ‘WMO’ imefafanua kuna uwezekano wa asilimia 66 kwamba wastani wa joto duniani karibu na uso wa dunia kati ya mwaka 2023 na 2027, utakuwa zaidi ya nyuzi joto 1.5°C juu ya viwango vya kabla ya maendeleo ya viwanda.
WMO imefafanua katika taarifa hiyo “kuongezeka kwa joto kunakosababishwa na matukio ya mfumo wa hali ya hewa wa El Nino kunatarajiwa kuendelea katika miezi ijayo. Ongezeko la joto pia limesababishwa na mabadiliko ya tabianchi yanayochochewa na binadamu.”
Petteri Taalas Katibu Mkuu wa WMO amesema “Hali hii itakuwa na madhara makubwa kwa afya, uhakika wa chakula, usimamizi wa maji na mazingira. Tunahitaji kujiandaa.”
Kwa kawaida, El Niño huongeza viwango vya joto duniani mwaka mmoja baada ya kutokea, katika hali hii, hiyo inamaanisha ni mwaka 2024.
Ili kuzuia uchafuzi wa mazingira unaosababisha ongezeko la joto duniani, Mapatano ya Tabianchi ya Paris yalifikiwa katika fremu ya Kongamano la Mfumo wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (UNFCC). Nchi 197 ziliidhinisha mapatano hayo tarehe 12 mwezi Disemba mwaka 2015 mjini Paris.
Hata hivyo katika hatua ya kukaidi jamii ya kimataifa, Marekani ambayo inaongoza katika kuchafua mazingira ya dunia na hivyo kusababisha joto kali ilijiondoa katika mkataba huo wa Paris wa kulinda mazingira.