MKUU wa Mkoa wa Tabora, Dk Batilda Burian amelishukuru Shirika la World Vision Tanzania kwa kutoa elimu kwa watoto na kuongeza ufaulu kutoka asilimia 61 hadi kufikia 81 kwa shule za msingi na sekondari wilayani Igunga mkoani Tabora.
Kauli hiyo ilitolewa jumatano na mkuu huyo wa mkoa wakati wa makabidhiano ya mradi wa maendeleo kwa wananchi wa Kata ya Manonga wilayani humo.
Balozi Dk Burian alisema licha ya kuongeza ufaulu huo pia wamefanikiwa kupunguza tatizo la mimba za utotoni.
Pamoja na pongezi alilihakikishia shirika hilo kwamba serikali itaendelea kusimamia kikamilifu miradi yote iliyoanzishwa na kuitekeleza katika kipindi chote walichokaa wilayani Igunga.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu, Godfrey Kisemba wakati wa makabidhiano Tarafa ya Manonga wilayani humo, alisema Shirika hilo limefanyakazi na jamii kwa miaka 18 tangu mwaka 2004.
Kasembe alisema kwamba kabla ya kuanzishwa kwa mradi huo, utafiti wa awali ulifanyika mwaka 2004-2005 kwa lengo la kubaini changamoto zilizokuwepo katika jamii na kubaini changamoto katika sekta ya kilimo, afya, elimu na uchumi.
Aidha, alisema Shirika la World Vision kupitia ufadhili kutoka Canada kwa kushirikiana na serikali na jamii wakiwemo wadau mbalimbali walifanikiwa kutatua changamoto zilizokuwepo na kuwajengea uwezo wakulima kwa kuwapa mafunzo ya kilimo bora cha mpunga na kuwezesha mifereji ya maji ya umwagiliaji.
Alisema wakulima hao wameweza kuongeza uzalishaji wa mahindi kutoka gunia 6 za kilo 100 kwa ekari na kufikia gunia 15 baada ya kujengewa uwezo kwa kutumia pembejeo na mbegu bora.
Kasembe alisema mafanikio mengine ni kujenga ghala bora la kuhifadhia mazao baada ya kuvuna ili kuongeza thamani na kupunguza upotevu utokanao na mazingira duni ya kutunzia.
Aidha, World Vision Tanzania imewezesha ustawi wa watu 5,059 kwa kuwapatia huduma ya maji, matundu ya vyoo na kuwezesha vikundi mbalimbali kuanzisha vikundi vya kuweka na kukopa.
Shirika hilo limewataka wananchi kutunza na kuifanya endelevu miradi ya miundombinu ambayo lengo lake ni kuikomboa jamii inayoishi katika maeneo ya Manonga wilayani Igunga mkoani Tabora.