World Vision yafanya kweli ufugaji Mufindi

SHIRIKA la World Vision Tanzania, limetenga Sh Bilioni 1.4 kuwawezesha wananchi wa vijiji saba vya kata ya Maduma na Nyololo wilayani Mufindi mkoani Iringa kunufaika na mradi wa ufugaji wa ng’ombe wa maziwa, nguruwe na kuku.

Kwa kupiti mradi huo (Nyololo Animals Gift Project) uliozinduliwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki; ng’ombe wa maziwa 300, nguruwe 600 na kuku 400 watanunuliwa na kuwanufaisha zaidi ya wananchi 3600 kwa ujumla wake, huku 1200 kati yao wakinufaika moja kwa moja.

Mkurugenzi Mwandamizi wa Shirika la World Vision Tanzania Dk Joseph Mayala alisema mradi huo utakaoinua kipato na maisha ya wananchi unalenga kuboresha mnyololo wa thamani ya ufugaji kwa kuchochea pia kilimo cha mazao ya bustani kupitia makundi ya mbogamboga kwa ajili ya uboreshaji wa lishe.

Mayala alisema mradi huo utashirikisha wataalamu wa kilimo na mifugo, viongozi wa serikali ngazi ya kata na vijiji, na kuwatambua wanufaika watakaokuwa na sifa ya kusimamia na kuendesha miradi ya ufugaji kwa kuzingatia vigezo vitakavyowekwa.

Alisema mradi huo lazima ujenge misingi bora ya kuinua kipato kwa kushirikiana na serikali na wadau wengine na kuhakikisha una mchango kwenye ulinzi wa mtoto dhidi ya ukatili.

Akizindua mradi huo, Waziri wa Mifugo na Uvuvi alisema kuanzishwa kwa mradi huo kumeleta neema nyingine kwa wananchi wa kata hizo kwa kuanzisha kituo cha kukusanyia maziwa, kujengwa kwa majosho mawili ya kuogeshea ng’ombe na kuchimbiwa visima vya maji kwa wananchi wa vijiji vinavyozunguka mradi.

Waziri aliwataka viongozi wa World Vision kufika wizarani kuchukua mbegu za chakula cha mifugo na kuwafundisha wananchi namna ya kulima na kuvuna malisho hayo kwa kuwa serikali tayari ina mbegu hizo.

Alisema serikali imedhamiria kuona wafugaji wanafuga kisasa  kwa kufuga ng’ombe wachache kwa tija zaidi ili kuwasaidia kukuza uchumi wao na maendeleo yao.

Aidha Waziri Ndaki alisema serikali kwa kushirikiana na shirika hilo watatafuta ng’ombe dume kumi bora, ili kuwawezesha wafugaji wa kata hizo kupandikiza kwa gharama nafuu tofauti na ilivyo hivi sasa.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Saad Mtambule aliwataka wanufaika wa miradi ya World Vision kutoa ushirikiano wa kutosha na kuitunza miradi hiyo ili kuleta manufaa makubwa zaidi.

Mtambule alisema kuwa mradi huo unakwenda kutatua tatizo la lishe kwa wananchi wa wilaya hiyo na kuwaondolea udumavu ambao umekuwa unawatesa kwa muda mrefu

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x