Wydad Vs Simba hesabu ngumu

MOROCCO: Wawakilishi wengine wa Tanzania katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba watatupa karata yao muhimu usiku wa leo nchini Morocco dhidi ya Wydad Casablanca.
Mchezo huo ni watatu kwa timu zote mbili huku kila upande ukitafuta pakutokea kutokana na matokeo yasiyoridhisha katika michezo miwili iliyopita, ambapo bado timu hizo hazijaonja ladha ya ushindi kwenye mitanange hiyo.
Wydad ambao ni wanafainali wa michuano ya msimu uliopita wapo kwenye shinikizo kubwa wakiwa wametandikwa michezo yote miwili na kama watashindwa kufurukuta mbele ya mnyama Simba basi shughuli yao itakuwa ngumu mno kusalia kwenye michuano hiyo.
Kwa upande wa Simba wamesajili sare katika michezo yote miwili waliyocheza, ushindi katika mchezo wa leo utarejesha tena imani kwa wanazi wa timu hiyo.
Ikumbukwe sio mara ya kwanza timu hizo kukutana kwani msimu uliopita zilikutana katika mchezo wa robo fainali ya michuano hiyo ambapo kila timu ilishinda mchezo wa nyumbani kwa uwiano wa bao1-0 na kisha Wydad akasonga mbele kwa mikwaju ya penati.
Mchezo huo utaanza saa nne usiku katika Uwanja wa Marrakech.
2 comments

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *