MAKUMBUSHO ya Taifa Dar es Salaam, imehifadhi magari sita yaliyotumiwa na Mwalimu Nyerere Julius Nyerere, wakati wa uhai wake, likiwemo gari ambalo lilitumika katika awamu tatu za uongozi.
Mhifadhi wa Makumbusho, Pius Gondeka amesema magari yote kila moja lina historia yake, likiwemo gari aina ya Rolls Royce, ambayo ni gari la gharama ilitengenezwa Uingereza mwaka 1938 na lilifika Tanganyika mwaka 1962, lilitumiwa na viongozi mbalimbali katika shughuli za kiserikali.
Amesema gari hiyo ilitumika kupokea wageni mashuhuri mbalimbali waliokuwa wakija kumuona Mwalimu Nyerere na kutembelea Tanganyika.
Amewataja baadhi ya viongozi waliofika na kulitumia gari hilo ni pamoja na Mfalme wa Ethiopia, hayati Haille Selasie, Rais wa Liberia, William Tubman, Gavana wa mwisho Sir Richard Turnbull.
Amesema alilitumia katika shughuli za kiserikali na mwaka 1978 Mwalimu Nyerere aliagiza gari hilo kupelekwa Makumbusho likitokea Ikulu.
Gondeka amesema gari nyingine ni aina ya Rolls Royce (Phantom V), ambayo ilitumiwa na Mwalimu Nyerere mwaka 1970 kuwapokea viongozi wa nchi mbalimbali walioitembelea Tanzania.
Amesema gari hilo limetumiwa pia na Rais wa Awamu ya Pili, Mzee Ali Hassan Mwinyi na Rais wa Awamu ya Tatu, hayati Benjamin Mkapa.
Gondeka amesema gari hilo lina sehemu mbili za kuweka bendera mbele, ambapo upande wa kulia anakaa Rais mgeni aliyewasili na kuwekwa bandera ya nchi yake na kwa upande wa kushoto anakaa Rais mwenyeji na bendera ya Tanzania.

Anasema sehemu ya juu ya gari inaweza kufunguliwa na kuwa wazi, endapo viongozi watasimama kusalimia ama kupunga mikono kwa wananchi.
“Gari hiyo ilipendwa sana kwa wakati ule, ndio gari ilionekana ina nguvu zaidi, gari ya hadhi, heshima na kuonesha kujali wageni,” amesema.
Pia amesema lipo gari la mwisho lililotumiwa na Mwalimu Nyerere kabla ya kufikwa na mauti, ambalo lilimpeleka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa, Dar es Salaam, kueleka hospitali ya St. Thomas Uingereza kwa matibabu, ambako alifariki dunia Oktoba 14, 1999.
Amesema gari hilo, aina ya Mercedes Benz E 300, limetengenezwa Ujerumani na kununuliwa na serikali ya Tanzania, Desemba 17, 1996 na kwamba lilitumiwa na Mwalimu Nyerere katika shughuli mbalimbali, hususani katika Jiji la Dar es Salaam, baada ya kustaafu.
Amesema gari hiyo ni ya mwisho kutumiwa na Mwalimu Nyerere kipindi cha uhai wake.
“Kwa mara ya mwisho gari hyo ilitumiwa na Mwalimu Agosti 31, 1999 alipotoka nyumbani kwake Msasani kwenda Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, tayari kwa safari ya London, Uingereza kupata matibabu,” amesema.
Amesema Baba wa Taifa alifariki Oktoba 14,1999 nchini Uingereza na Septemba 24, 2004 mjane wa Baba wa Taifa, Mama Maria Nyerere aliitoa gari hiyo kwa Makumbusho ya Taifa.
Gondeka amesema gari nyingine ni Mercedes-Benz 230.6, ilitumika katika shughuli za serikali, wakati wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), ilipoanza mwaka 1967 na kuvunjika mwaka 1977 kwa sababu mbalimbali.
Amesema upekee wa gari hilo ni kuwa liliweza kubeba marais wawili kwa wakati mmoja, Makamu wa Rais na mwandishi wa Rais ina sehemu tatu kwa ndani.
Pia amesema kuna gari aina ya Austin Morris (A40 Van Guards) maarufu kama Van Guards, ambayo ilitengenezwa Uingereza kati ya mwaka 1945 -1950, ambayo aliitumia katika shughuli za chama cha TANU na harakati za kudai Uhuru.
Gari lingine lililotumika wakati wa harakati za kupigania uhuru ni pamoja na aina ya Austin Morris (Minor), ambayo ilitengenezwa nchini Uingereza katika ya mwaka 1940-1950