JUMANNE iliyopita, aliyekuwa Rais Mteule wa Kenya, William Ruto aliapishwa kuwa Rais wa Tano wa nchi hiyo baada ya uchaguzi mkuu uliofanyika Agosti 9, mwaka huu kutokana na Uhuru Kenyatta kumaliza muda wake.
Miongoni mwa marais waliohudhuria hafla hiyo iliyofanyika jijini Nairobi, ni pamoja na marais wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) yaani Tanzania, Burundi, Rwanda, Sudan Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Uganda.
Katika sherehe hizo, Mwenyekiti wa EAC ambaye pia ni Rais wa Burundi, Evariste Ndayishimiye, alisema matarajio yake ni kuwa kuapishwa kwa Ruto kuiongoza Kenya kutachochea ushirikiano miongoni mwa nchi za jumuiya hiyo na kuipa maendeleo zaidi.
Rais wa Uganda, Yoweri Museveni alisisitiza suala la jumuiya hiyo kuimarisha mtangamano na uzalishaji mali kupitia kilimo biashara, huduma, teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama) na nyingine zikiwamo huduma za hoteli ili kuongeza ajira na kukuza uchumi wa nchi.
Museveni alisema wakati yote hayo yanafanyika, nchi za EAC hazina budi kuzingatia kuwa, ili kukua kiuchumi na hata kufikia au kukaribia kufikia mataifa yaliyoendelea kiuchumi duniani, hapana budi kujenga na kuimarisha kwanza soko la kanda hii.
Kwetu sisi, suala la kukuza na kuimarisha soko la bidhaa na huduma ndani ya EAC kama alivyosema Museveni, linapaswa kuwa moja ya vipaumbele vya jumuiya kwa kuhakikisha kunakuwa na amani ya kutosha na pia nchi zenye sifa kadiri ya vigezo, zinajiunga katika safari hiyo.
Kujiunga kwa wanachama wapya wenye sifa kama ilivyokuwa hivi karibuni kwa nchi ya DRC, kuna maana kubwa katika jumuiya kwa kuwa kunaongeza walaji (soko) na hivyo, kuongeza ajira kupitia walaji hao wa huduma na bidhaa zinazozalishwa na kutolewa ndani ya EAC.
Yote haya yatawezekana zaidi nchi za EAC zitakapozingatia kwa dhati suala la uhusiano mwema, amani na usalama.
Hili ndilo lilimfanya Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania kusema kuwa, kama kuna kitu ambacho Wakenya wamekifanya na kuwa zawadi kwa EAC mwaka huu, ni suala la Wakenya kuanza, kufanya na kumaliza mchakato wa uchaguzi mkuu kwa amani.
Rais Ruto, kabla na baada ya kuapishwa, alisema miongoni mwa mambo atakayotilia nguvu ni kuhakikisha nchi yake inashirikiana na kuhusiana vyema na wanachama wa EAC katika nyanja mbalimbali za kiuchumi, kisiasa, kiulinzi, kijamii na kiutamaduni.
Tunaunga mkono misimamo iliyotolewa na viongozi hao wa EAC kwa niaba ya wenzao kwa kuwa, umoja ni nguvu na pia hakuna nchi au jamii yoyote duniani inayopata maendeleo kama imejitenga na haina amani na usalama.
Ndio maana tunasema, yaliyosemwa na marais kuhusu soko na kuimarika kwa EAC yazingatiwe na nchi zote wanachama ili muungano wa EAC uzae matunda tarajiwa.