Yanayopaswa kufanyika mtu ateuliwe kuwa mgombea

UCHAGUZI ni mchakato wa watu kumchagua mtu au watu watakaojaza nafasi kwenye ofisi ya umma ili kuwawakilisha katika ngazi mbalimbali za maamuzi.

Kwa mujibu wa Encyclopedia Britannica uchaguzi ni mfumo rasmi unaohusisha mchakato wa kumchagua mtu kwa ajili ya kushika nafasi kwenye ofisi ya umma au kukubali au kupinga pendekezo la kiutawala (political proposal) kwa kupiga kura.

Uchaguzi katika mfumo wa utawala unaweza kutumika kujaza nafasi kwenye Bunge, serikali kuu, mikoa na serikali za mitaa. Kwa muktadha wa Tanzania, uchaguzi haswa wa kujaza nafasi kwenye utawala wa umma ngazi ya kata, jimbo na urais unaratibiwa, kusimamiwa na kuendeshwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Ili kuhakikisha kwamba kunakuwa na ushindani uliosawia, huru na wa haki, Tume inahakikisha kwamba mchakato wote kuanzia ngazi ya uteuzi wa wagombea, kampeni na hata siku ya kupiga kura unasimamiwa na kuratibiwa kikamilifu.

Hivi karibuni, Tume imetangaza nafasi wazi ya ubunge katika Jimbo la Amani, Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi, Zanzibar na kata 12 za Tanzania Bara ambapo kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyosainiwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume, Dk Wilson Mahera wagombea watachukua fomu kuanzia Novemba 24 hadi 30, 2022, siku ya uteuzi itakuwa Novemba 30, 2022, kampeni zitafanyika kuanzia Desemba 01 hadi 16 mwaka huu (2022) na siku ya uchaguzi itakuwa Desemba 17, mwaka huu.

Kata zilizotangazwa kufanya uchaguzi mdogo na halmashauri zilizopo kwenye mabano ni Majohe (Jiji la Dar es Salaam), Dabalo (Chamwino), Ibanda (Kyela), Mndumbwe (Tandahimba), Njombe Mjini (Mji wa Njombe), Misugusugu (Mji wa Kibaha), Dunda (Bagamoyo), Mwamalili (Manispaa ya Shinyanga), Mnyanjani (Jiji la Tanga), Lukozi (Lushoto) na Vibaoni (Mji wa Handeni).

Ifahamike kwamba katika ngazi ya uteuzi wa wagombea NEC kwenye tarehe iliyopangwa itafanya uteuzi wa wagombea wa uchaguzi ambao wamependekezwa na vyama vyao na watatakiwa kuwasilisha fomu za uteuzi katika ofisi za Wasimamizi wa Uchaguzi kwenye maeneo yao kabla ya muda uliopangwa siku hiyo ya uteuzi.

Ili kuepuka makosa ambayo yanaweza kumnyima mgombea fursa ya kuteuliwa kwa kuwasilisha Tume fomu iliyokosewa au ambayo haijakidhi vigezo vya kuteuliwa, mgombea anapewa fursa ya kupeleka fomu yake kwa msimamizi wa uchaguzi siku tatu kabla kwa ajili ya kukaguliwa na kuona kama fomu yake imekidhi vigezo na masharti yaliyowekwa kwa mujibu wa sheria.

Mada hii ni muhimu kufahamika vizuri haswa katika kipindi hiki ambapo taifa linashuhudia chaguzi ndogo kwenye maeneo mbalimbali ya nchi kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo za wabunge na madiwani kujiuzulu, kuhama vyama na wengine kufariki. Kwa kuwa chaguzi hizi ndogo zinahusisha wabunge na madiwani makala haya itaangazia zaidi taratibu za kufuatwa katika teuzi za wagombea kwa nafasi hizo.

Kwa nafasi ya mgombea wa kiti cha ubunge, Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo anao wajibu wa kumteua mgombea wa nafasi ya Ubunge baada ya kujiridhisha kuwa Fomu ya Uteuzi Na. 8B na Fomu Na. 10 ya kuheshimu na kuzingatia maadili ya uchaguzi zimejazwa kikamilifu.

Fomu Na. 8B inapaswa kujazwa kwa herufi kubwa lakini ni jina moja tu ndilo linapaswa kuandikwa kwa herufi kubwa kwenye karatasi ya kupiga kura kwa hiyo mgombea anapaswa kujaza mwanzoni jina analopendelea liandikwe kwa herufi kubwa kwenye karatasi ya kupigia kura likifuatiwa na majina mengine.

Ni muhimu kujua kwamba baadhi ya wagombea huwawekea wenzao pingamizi haswa wanapoona kwamba mgombea ameandika majina yake kwa kutofuata mtiririko, jambo hili kwa mujibu wa sheria si kosa na halimnyimi mgombea sifa za kuteuliwa.

Kwenye fomu hiyo majina ya wadhamini yanapaswa kujazwa kwenye jedwali na baada ya hapo fomu inapaswa kuwasilishwa kwa msimamizi wa uchaguzi pamoja na picha nne za mgombea za rangi (passport size). Pia fomu hiyo inapaswa kuwasilishwa pamoja na Fomu Na. 10 ya tamko la mgombea la kuheshimu na kutekeleza maadili ya uchaguzi.

Ili fomu hiyo ikamilike kwa ajili ya uteuzi inapaswa pia kuambatanishwa na uthibitisho wa chama cha siasa wa kumpendekeza mgombea ubunge, tamko la wadhamini, tamko la kisheria la mgombea ubunge na baada ya hapo itakamilishwa kwa kupata uthibitisho wa msimamizi wa uchaguzi.

Utaratibu wa kukata rufaa kwa mgombea ubunge upo kwa mujibu wa sheria, Kifungu cha 40 (6) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343, kinatoa fursa kwa mgombea ambaye hakuridhishwa na uamuzi wa Msimamizi wa Uchaguzi kukata rufaa Tume. Uamuzi wa NEC kuhusu rufani hiyo utakuwa wa mwisho na hautahojiwa katika mahakama yoyote.

Kifungu hicho kinatoa fursa kwa asiyeridhika na uamuzi wa Tume kufungua malalamiko ya uchaguzi mahakamani baada ya matokea ya uchaguzi wa wabunge kutangazwa. Baada ya uteuzi wa mgombea upande ambao haujaridhika unaweza kukata rufaa kwa kujaza Fomu Na. 12.

Kwa upande wa mgombea wa udiwani, uteuzi kwa mujibu wa kanuni ya 25 (4) ya Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa (madiwani) hufanywa na msimamizi wa uchaguzi wa jimbo au msimamizi msaidizi wa uchaguzi baada ya kujiridhisha kuwa mgombea amejaza kikamilifu Fomu Na. 8C ya uteuzi na Fomu Na. 10 ya kuheshimu na kuzingatia maadili ya uchaguzi.

Masharti na mtiririko wa ujazaji unafanana na ule wa mgombea ubunge isipokuwa mgombea ubunge anaweka dhamana ya Sh 50,000 na mgombea udiwani anaweka dhamana ya Sh 5,000.

Utaratibu wa pingamizi dhidi ya mgombea udiwani upo kwa mujibu wa Kifungu cha 44 (3) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292, pingamizi kwa mgombea udiwani huwekwa na mgombea mwingine wa nafasi ya udiwani au Msajili wa Vyama vya Siasa au msimamizi wa uchaguzi kupitia Fomu Na. 9C. Pingamizi husikilizwa na kuamuliwa na msimamizi msaidizi wa uchaguzi.

Msimamizi msaidizi wa uchaguzi ngazi ya kata baada ya kupokea pingamizi na kufanya uamuzi anatakiwa amfahamishe msimamizi wa uchaguzi juu ya uamuzi huo ili aupitie na kuona kama umezingatia sheria au la. Msimamizi wa uchaguzi ana mamlaka ya kubadili uamuzi huo kama itabainika kuwa haukuzingatia matakwa ya kisheria.

Kifungu cha 44 (5) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292, kinaruhusu wagombea kukata rufaa NEC kupinga uamuzi wa msimamizi wa uchaguzi kuhusu pingamizi dhidi ya mgombea.

Mwandishi wa makala haya ni Ofisa Habari Mwandamizi, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x