VINARA wa Ligi Kuu Bara, Yanga wanatarajiwa kushuka dimbani leo dhidi ya wenyeji Azam FC katika mchezo wa mzunguko wa 18 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Timu hizo katika mchezo wa mzunguko wa kwanza zilitoka sare ya mabao 2-2 kwenye uwanja huohuo, mchezo uliokuwa na ushindani mkali na sasa wanakutana tena bado wote ni bora ila wametofautiana vitu vichache.
Kitu walichotofautiana ni pointi Yanga inaongoza kwa pointi 44 na Azam FC iko nafasi ya tatu kwa pointi 37, kuna tofauti ya pointi saba.
Yanga ni bora katika safu ya ushambuliaji ikiongoza kwa kufunga mabao 33 ikiruhusu kufungwa mabao manane kwenye ulinzi huku Azam FC ikifunga mabao 25 na kuruhusu 16 ikionesha wazi kwenye ulinzi kuna shida.
Ni mchezo wenye presha kwa timu zote mbili kwasababu Yanga itataka kushinda kulinda nafasi yake ya kuongoza na kuwa rahisi kutetea taji lakini pia, wenyeji Azam FC wametoka kupata sare mbili mfululizo katika michezo iliyopita ambayo imewapunguza kasi wanahitaji kushinda ili kutoachwa mbali kwa pointi kwa kuwa bado wapo kwenye mbio za kuwania taji.
Timu hizi mara nyingi zinapokutana kila moja hucheza soka la kiwango cha juu kuonesha ni bora kuliko mwingine. Kila mmoja ana kila sababu ya kushinda na kila mmoja ana wachezaji wazuri wenye uwezo hivyo, huenda ukawa mchezo wenye ushindani mkali.
Kocha Msaidizi wa Yanga Cedric Kaze alisema wachezaji wake wote wako salama na tayari kupigania pointi tatu ingawa anaamini unaweza kuwa wenye presha kwa kila mmoja.
“Tunajua Azam wana winga zenye kasi lakini kuna maeneo mengine hawako vizuri. Sisi tumejiandaa vizuri kuendelea kuonesha kiwango cha juu, wachezaji wamejiandaa vya kutosha, tunaamini watacheza kwa kiwango kikubwa,”alisema.
Kwa upande wake, Kocha Msaidizi wa Azam FC Idd Abubakar alisema “tunajua Yanga ni timu kubwa na Azam pia, ni wakubwa na sote tuna malengo ya kuchukua taji, ni dhahiri mechi haiwezi kuwa nyepesi kutokana na ukubwa wa timu zote kwani presha imeshakua juu,”
Michezo mingine leo ni kati ya Mbeya City dhidi ya Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya na Kagera Sugar itakuwa mwenyeji wa Geita Gold kwenye Uwanja wa Kaitaba, mkoani Kagera.