LIGI Kuu Tanzania Bara inatarajiwa kuendelea tena Jumanne ambapo mabingwa watetezi, Yanga watakuwa wenyeji wa Azam kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Ligi imerejea baada ya kusimama kwa takribani wiki tatu kupisha timu ya taifa.
Mchezo huo unasubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa pande zote mbili kutokana na maboresho ya vikosi vyao katika usajili.
Yanga wamedhamiria kuendeleza rekodi yao ya kuifunga Azam FC kama ilivyokuwa msimu uliopita ambapo walishinda mechi zote mbili za ligi na kuchukua pointi sita ambazo zilichangia kwa kiasi kikubwa kubeba ubingwa baada ya kumaliza misimu minne bila taji.
Mbali na rekodi ya kushinda mechi zote mbili za msimu uliopita, Yanga leo inaingia uwanjani ikiwa na kumbukumbu nzuri ya kuanza vyema msimu huu baada ya kushinda mechi mbili za awali wakati wapinzani wao Azam FC wamekusanya pointi nne katika mechi mbili baada ya kushinda mchezo mmoja na kutoka sare moja.
Kikosi cha Azam kinaingia katika mchezo huo bila Kocha Mkuu, Abdulihamid Moallin ambaye amefutwa kazi baada ya uongozi wa timu hiyo kutoridhishwa na mwenendo wa timu hiyo katika mechi mbili zilizopita na kwa sasa kocha wa washambuliaji, Kally Ongala ndio anakiongoza kikosi hicho kwa muda.
Pamoja na mapungufu hayo lakini mchezo huo bado unatarajiwa kuwa mgumu na wenye ushindani mkali hiyo ni kutokana na uimara wa vikosi vyote viwili kutokana na mabadiliko makubwa ya wachezaji.
Lakini pamoja na hilo wenyeji Yanga wanapewa nafasi kubwa ya kuondoka na pointi tatu kutokana na namna kocha wake, Nasreddine Nabi alivyokiandaa kikosi chake na namna ya kuwatumia wachezaji wapya na wa zamani aliokuwa nao kwenye timu yake.
Ingizo kama la Benard Morison na Aziz KI, linatishia amani kwa Azam kutokana na uwezo waliokuwa nao wachezaji hao katika mechi zilizopita lakini ubora aliokuwa nao mshambuliaji, Fiston Mayele, mabeki wa Azam kina Daniel Amoah na Malik Ndoyo raia wa Senegal wanapaswa kuwa makini muda wote.
Kocha Nabi, amekiri kuwa huo ni mchezo mgumu kwao kutokana na uimara wa kikosi cha Azam kwa kufanya usajili mkubwa ambao kwa kiasi kikubwa umekibadilisha kikosi chao.
“Tunakwenda kukutana na Azam ya tofauti na ile ambayo tulicheza nayo msimu uliopita, nimewaona mechi zao nyingi wamesajili wachezaji wenye vipaji na wanaohitaji kuchungwa, hatupaswi kuwadharau kutokana na matokeo yao tutaingia kwa kuwaheshimu kama wakubwa wenzetu lakini lengo letu ni pointi tatu,” alisema Nabi.
Alisema wakati ligi imesimama alikitumia kufanya mazoezi ya nguvu na kuziimarisha sehemu ambazo zilionesha mapungufu kwenye mechi zilizopita kupitia mechi ya kirafiki, anaamini kila kitu kimekaa sawa kwa ajili ya mchezo huo wa leo na mechi nyingine zijazo.
Kwa upande wake Kally alisema wamekamilisha maandalizi yote ikiwemo kuchagua wachezaji kwa ajili ya mchezo huo aliouita ni wa kulipa kisasi.
Kally amekiri kuwa Yanga ni timu bora kwa sasa na wanakikosi bora lakini hilo haliwafanyi kuhofia kupeleka timu uwanjani, wamejipanga kuhakikisha wanamaliza uteja kwa kuifunga Yanga na kurudisha furaha kwa mashabiki wao.
“Maandalizi yetu yamekamilika na tunasubiri muda wa mchezo, najua Yanga ni timu kubwa imesajili vizuri na ndio mabingwa watetezi lakini kwa ubora wa kikosi chetu naamini tunao uwezo wa kuwachalenji na imani yangu naamini tutapata ushindi,” alisema Kally.
.