Yanga haizuiliki

YANGA imeendelea vema na kampeni za kutetea taji la Ligi Kuu baada ya kushinda mabao 2-0 dhidi ya Dodoma Jiji kwenye Uwanja wa Liti mkoani Singida jana.

Mabao yote mawili yalifungwa na Fiston Mayele akifikisha mabao manane na kuongoza katika orodha ya wafungaji bora.

Ushindi huo unaifanya Yanga kupanda tena katika uongozi wa ligi kwa uwiano mzuri wa mabao wakifikisha pointi 29  sawa na Azam FC iliyo nafasi ya pili.

Lakini huenda ikaongoza kwa muda mfupi kwani wekundu wa Msimbazi, Simba wanaweza kupanda kutoka nafasi ya tatu hadi ya kwanza kama watashinda mchezo wao wa leo dhidi ya Mbeya City watafikisha pointi 30.

Aidha, Dodoma Jiji hali inazidi kuwa mbaya kwani matokeo hayo yamewashusha nafasi moja chini kutoka ya 14 hadi 15 ikibaki na pointi tisa katika michezo 12.

Katika mchezo huo Dodoma ilicheza kwa tahadhari ikionekana kulinda lango na kushambulia kwa kushtukiza pale ilipopata nafasi lakini dakika ya 41 walishindwa kumzuia Mayele aliyemalizia wavuni mpira kwa mguu wa kulia baada ya kupata pasi nzuri ya Tuisila Kisinda.

Dakika ya 67 baadaye alifunga tena bao baada ya kupata pasi ya Denis Nkane.

Yanga kama ingetulia ingeondoka na ushindi zaidi ya huo kwani ilitengeneza nafasi nyingi na kushindwa kuzitumia. Pia, Dodoma Jiji walitengeneza nafasi zaidi ya mbili nao walikosa ufanisi mzuri katika kumalizia.

Beki wa Yanga, Bakari Mwamnyeto alitolewa mapema dakika ya 39 baada ya kuumia na nafasi yake ilichukuliwa na Ibrahim Bacca.

Habari Zifananazo

Back to top button