KLABU ya Yanga imeeleza kuwa itatumia Uwanja wa Azam Complex unaomilikiwa na klabu ya Azam FC kama uwanja wao wa nyumbani baada ya Uwanja wa Mkapa kuwa kwenye marekebisho.
Akizungumza na waandishi wa habari mapema hii leo, Ofisa Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ali Kamwe amesema wataanza kutumia uwanja huo kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho la Azam dhidi ya Tanzania Prison Ijumaa hii.
“Kuanzia sasa hivi mchezo huo wa shirikisho na mechi za ligi zinazofuata tutatumia Azam Complex kama uwanja wetu wa nyumbani.” Amesema Ali Kamwe.
Kuelekea mchezo wa Kombe la Shirikisho Barani Afrika, Kamwe amesema kesho timu hiyo itazindua kampeni maalumu za hamasa kwa mashabiki ili kujitokeza kwa wingi katika mchezo wao dhidi ya Real Bamako utakaochezwa Machi 8, 2023.
“Kesho majira ya saa 7 mchana maeneo ya Buguruni Chama viongozi wetu wanakwenda kuzindua hamasa ya kuitafuta shangwe ya tarehe 8, tutakuwa na tukio kubwa lililoandaliwa na viongozi wetu wa mkoa.” Amesema Kamwe.