Yanga, Mayele bado wavutana

HATIMA ya mchezaji, Fiston Mayele kuondoka au kuendelea kuitumikia Yanga msimu ujao inatarajiwa kujulikana Jumatatu ijayo.

Kiwango kilichooneshwa na Mayele msimu huu ambapo aliiwezesha Yanga kutetea makombe yake na kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika kimeonekana kuzivutia klabu kutoka mataifa mbalimbali zikitaka huduma yake.

Mayele aliibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu Soka Tanzania Bara ambapo alifunga mabao 17 akifungana na Saido Ntibanzonkiza wa Simba lakini pia aliibuka mfungaji bora wa Kombe la Caf kwa kufunga mabao saba na kuisaidia Yanga kufika fainali ya michuano hiyo ya pili kwa ukubwa ngazi ya klabu Afrika.

Akizungumzia mustakabali wake mfumania nyavu huyo wa kimataifa wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) alisema mpaka Jumatatu itajulikana kama anasalia au anaondoka Yanga.

“Nina kikao na uongozi wa timu Jumatatu, nadhani baada ya kikao hicho kila kitu kitajulikana lakini niseme ukweli mimi bado ni mchezaji wa Yanga kwa sababu bado nina mkataba wa mwaka mmoja na hata haya mafanikio na umaarufu niliokuwa nao ni Yanga ndio wamenipatia, kwa hiyo siwezi kuwadharau,” alisema Mayele.

Alisema kama ikitokea wameshindwana na uongozi wa Yanga ataondoka na kwenda kujiunga na timu nyingine nje ya Tanzania na anafanya hivyo kwa kulinda heshima kwa viongozi na mashabiki wa Yanga.

“Nimekuja hapa nikiwa sijulikani lakini klabu imenipokea vizuri, viongozi na mashabiki wakanipa ushirikiano wa kutosha, tumeishi kama ndugu, ninafuraha kuwa Yanga ila acha tuone kikao cha mwisho tutafikia wapi, kama nitabaki au nitaondoka,” alisema Mayele.

Katika kikao cha mwisho inaelezwa kuwa Yanga walimpa Mayele ofa ya mshahara wa dola 12,000 ambazo ni zaidi ya Sh milioni 28 za Tanzania kwa mwezi lakini Mayele na wakala wake wanataka mkataba wa mwaka mmoja kwa mshahara wa dola 15,000 ambazo ni zaidi ya milioni 35 za Tanzania kwa mwezi.

Katika hatua nyingine Yanga ilitoka sare ya bila kufungana na Nyasa Big Bullets katika mchezo wa kuadhimisha miaka 59 ya Uhuru wa Malawi, Lilongwe jana.

Habari Zifananazo

Back to top button