HISTORIA inaendelea kuandikwa na sasa huenda mguu mmoja ukawa umetangulia fainali, hivyo ndivyo unavyoweza kusema baada ya kikosi cha Yanga kushinda mabao 2-0 katika nusu fainali ya kwanza Kombe la Shirikisho Afrika iliyopigwa Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
Huwezi kuielezea furaha ya mashabiki wa Yanga mara baada ya Aziz Ki kufufua matumaini ya kunusa fainali kwa kupachika bao la kwanza dakika ya 64 kwa shuti kufuatia kazi nzuri ya Tuisila Kisinda.
Wakati mchezo ukiendelea dakika za mwishoni, Bernad Morrison hakufanya makosa baada ya kutumia vyema pasi ya Fiston Mayele na kuandika bao la pili lililowapa furaha maradufu wanajangwani.
Tafsiri ya ushindi huo ni mwanzo mzuri wa Yanga kuelekea mchezo wa fainali, licha ya ukweli kuwa wapinzani wao Marumo Gallants sio timu ya kubeza, hivyo kazi kubwa Yanga wanatakiwa kuifanya wiki ijayo huko Afrika Kusini.
Kwa kufunga mabao mawili, Yanga imelamba Sh milioni 20 ya Rais Samia kama sehemu ya ahadi yake ya kununua kila bao kwa Sh milioni 10 katika hatua hiyo hadi fainali.
Comments are closed.