Yanga: Mtasubiri sana
MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Bara Yanga wamerejea kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Kagera Sugar mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza jana.
Bao pekee la Yanga kwenye mchezo huo lilifungwa na mshambuliaji kinda wa timu hiyo, Clement Mzize dakika ya 18 akimalizia vema krosi iliyopigwa na beki wa kulia wa timu hiyo, Kibwana Shomari.
Mzize amecheza mchezo wake wa kwanza wa Ligi Kuu Bara tangu alipopandishwa kikosi cha wakubwa na kocha mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi.
Dakika ya 71 Kipa wa Yanga, Djigui Diara, aliibuka shujaa kwa timu yake baada ya kucheza mpira wa penalti uliopigwa na mshambuliaji wa Kagera Sugar, Erick Mwijage.
Yanga imefikisha michezo 46 ya Ligi Kuu Bara bila kupoteza tangu msimu uliopita wamerejea kileleni wakiwa na pointi 23 sawa na Azam FC, huku timu hizo zikipishana kwa idadi ya mabao ya kufunga na kufungwa.
Kagera Sugar wao wameshuka hadi nafasi ya 13 kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara wakiwa na pointi 11 baada ya kushuka uwanjani mara 11 wakishinda tatu, sare mbili na kupoteza mara sita.
Mchezo mwingine jana, Mbeya City ikiwa nyumbani imebanwa na kulazimishwa sare ya mabao 2-2 na Coastal Union mchezo wa Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.
Coastal Union walikuwa wa kwanza kupata bao dakika ya 24 lililofungwa na Greyson Gwalala, Mbeya City walisawazisha katika dakika ya 39 lililofungwa na Sixtus Sabilo.
Dakika ya 68 Hamad Majimengi aliongeza bao la pili kwa Coastal Union, Mbeya City walizinduka na kusawazisha bao hilo dakika ya 80 kwa mkwaju wa penalti uliofungwa na Sixtus Sabilo aliyefikisha mabao saba na kuwa kinara kwenye orodha ya wafungaji wa Ligi Kuu Bara.