Yanga, Singida kivumbi

Yanga

YANGA leo inakabiliwa na kibarua pevu cha kuikabili timu ya Singida Big Stars, katika mwendelezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, mchezo utakaofanyika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Timu hizo zinakutana zikiwa katika nafasi tofauti kwenye msimamo wa ligi, wenyeji Yanga wakiwa nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi hiyo wakikusanya pointi 23 katika michezo tisa wakati Singida Big Stars inashika nafasi ya nne kwenye msimamo ikiwa na pointi 18 wakicheza mechi 10.

Mchezo wa leo unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kutokana na ubora wa timu zote mbili msimu huu kuanzia kwenye usajili aina ya wachezaji wanaounda vikosi vyao na matokeo katika mechi walizocheza.

Advertisement

Timu hizo leo zinakutana kwa mara ya kwanza tangu Singida ilipoanza kushiriki Ligi Kuu msimu huu, ingawa Yanga inapewa nafasi kubwa ya kushinda kutokana na rekodi yake ya kucheza mechi 45 za ligi bila kupoteza hata mchezo mmoja.

Kocha msaidizi wa Yanga, Cedric Kaze ameeleza kuwa pamoja na kukosa muda wa kutosha wa kupumzika na kufanya mazoezi, lakini kikosi chao kipo tayari kwa ajili ya kuikabili Singida Big Stars leo.

Kocha huyo amesema anajua mchezo utakuwa mgumu kutokana na uzuri waliokuwa nao wapinzani wao Singida, lakini wamejipanga kukabiliana nao sababu kitu kizuri kilichopo kambini kwao ni ari ya upambanaji waliokuwa nayo wachezaji wao.

Kaze alisema katika mchezo wa leo watamkosa kipa wao namba moja, Djigui Diarra aliyeitwa kwenye timu ya taifa ya Mali pamoja na kiungo, Gael Bigirimana na Stephene Aziz Ki, aliyefungiwa kucheza mechi tatu na Bodi ya Ligi Kuu kwa kosa la kutopeana mikono na wachezaji wenzake katika pambano la watani wa jadi la Oktoba 23, 2022.

Kwa upande wake Kocha Mkuu wa Singida Big Stars, Hans Pluijm amekiri ugumu wa mchezo wa leo, lakini akasema wamejipanga kuhakikisha wanaidhibiti Yanga ili kupata ushindi mbele ya mabingwa hao watetezi.

Kocha huyo ameeleza kuwa pamoja na kuwahi kufanya kazi Yanga, lakini kwa sasa yeye ni mfanyakazi wa Singida na atahakikisha anapambana kupigania pointi tatu, ambazo zitawaweka katika nafasi nzuri kwenye msimamo wa ligi.

“Wachezaji wangu wote wapo fiti kuikabili Yanga na kila mmoja amepania kuhakikisha anacheza kwa kujitoa ili kupata ushindi mbele ya bingwa mtetezi Yanga,” alisema Pluijm.