Yanga, Singida zakamiana FA

LEO Yanga inashuka dimbani kwenye mechi ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (FA) dhidi ya Singida Big Stars, ikieleza uwezo na ari waliyonayo itawapa faida ya kuibuka na ushindi kwenye mechi hiyo itakayopigwa Uwanja wa Liti, Singida.

Singida Big Stars iliingia hatua hiyo baada ya kuitoa Mbeya City kwa kuwafunga mabao 4-1 wakati Yanga wakiitoa Geita Gold kwa ushindi wa bao 1-0.

Kuelekea mchezo huo, Kocha Msaidizi wa Yanga, Cedric Kaze jana alisema wanawaheshimu wapinzani wao kwa ubora walionao msimu huu, wakifahamu wanataka kuvuna chochote kwenye kombe hilo lakini wao wapo tayari kwa mapambano hayo.

Advertisement

“Tunaamini mchezo utakuwa mgumu zaidi ya ule tuliokutana kwenye ligi, hatutaki kujificha kwenye uchovu tulionao na kutafuta sababu, lakini kiakili tunaamini tuko vizuri, tunamheshimu mpinzani ameonesha kiwango kizuri lakini tutaweka nguvu zote kuhakikisha tunaenda fainali.

“Hamasa ni kubwa sana, siyo tu ya kuchukua makombe yote lakini kuchukua tena kombe hili tulilochukua mwaka jana, tumeona furaha yake kwa mashabiki na kwetu pia.

“Tunajua Singida haina cha kupoteza kwa sababu hii ni mechi ya mtoano lakini tupo tayari kwa hilo,” alisema Kaze.

Upande wa Kocha Mkuu wa Singida BS, Hans Pluijm alisema wanahitaji ushindi leo lakini wanafahamu uzuri, ubora wa kikosi wa timu wanayokutana nayo, akifahamu mbinu zao nyingi na wao wamejifua kukabiliana na hilo.

“Natumai tumejifunza makosa ya mechi ya mwisho ya nyumbani (dhidi ya Yanga) na hatutaki kuyarudia, Yanga ina kikosi imara na uwezo mkubwa na unapodhani umewakamata ndipo wanapokufunga.

“Hivyo tunahitaji umakini mkubwa kesho (leo), tunapaswa kuwa na umoja, nidhamu na kimbinu zaidi, tumejifunza mengi juu ya mechi hii, hatuwezi kueleza kila kitu jinsi tutakavyokwenda kucheza lakini tumejipanga dhidi ya Yanga,” alisema Pluijm.

Kuelekea mechi hiyo itakayopigwa kuanzia saa 9.30 alasiri, Singida itaingia ikiwa na kumbukumbu ya kufungwa mabao 4-1 na kisha 2-1 kwenye mechi mbili ilizokutana na Yanga kwenye ligi ingawa wamejinasibu kupambana kutofungwa tena.

Mshindi wa mechi hiyo atakutana na Azam FC kwenye fainali itakayopigwa Uwanja wa Mkwakwani, Tanga. Azam ilitinga fainali kwa kuifunga Simba bao 2-1.

1 comments

Comments are closed.