Yanga tayari Yanga tayari kuikabili Ihefu

YANGA leo inashuka kwenye Uwanja wa Highland Estate Mbarali, kukabiliana na wenyeji Ihefu FC katika mwendelezo wa mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara.
Timu hizo zinakutana zikiwa katika nafasi tofauti kwenye msimamo, Yanga wakiwa kileleni kwa kukusanya pointi 32 katika michezo 12 waliyocheza hadi sasa wakati Ihefu wapo nafasi ya mwisho wakikusanya pointi nane kwenye michezo 13 waliyocheza.
Yanga inaingia kwenye mchezo huo ikijivunia rekodi ya kushinda mechi sita mfululizo tangu ilipolazimishwa sare ya bao 1-1 na Simba Oktoba 23, wakati Ihefu inaingia kwenye mchezo huo ikitoka kupokea kichapo kutoka kwa Geita FC ikiwa ugenini.
Pamoja na udhaifu wa Ihefu, lakini mchezo wa leo unatarajiwa kuwa mgumu na wenye ushindani mkali kutokana na wenyeji kikosi chao kuundwa na wachezaji wazuri waliowahi kuchezea timu kubwa za Simba, Yanga na Azam FC, lakini hata kocha wake mkuu, Juma Mwambusi anawajua vizuri wageni wao.
Akizungumzia mchezo huo Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi ameeleza kuwa maandalizi yamekamilika na kikosi chake kipo tayari kwa mchezo huo ingawa ameendelea kulalamika ufinyu wa ratiba kuwa ngumu kwao kutokana na kukosa muda wa kupumzika.
Kocha huyo ameeleza kuwa anajua mchezo hautakuwa rahisi sababu Ihefu ni timu nzuri na ina wachezaji wenye uzoefu mkubwa na mbaya zaidi wachezaji weke wengi wamechoka kutokana na kucheza mfululizo. Kocha huyo amesema katika mchezo huo atawakosa wachezaji wawili ambao ni Feisal Salum na Bernard Morrison ambao wanakabiliwa na majeraha, lakini wachezaji wengine 22 aliokwenda nao Mbeya wote wapo tayari kwa mchezo huo.
Kwa upande wake kocha Mwambusi amekiri mchezo wa leo ni mgumu kwa kuwa wanacheza na timu bora kwenye ligi ya Tanzania lakini pamoja na yote wamejipanga kuhakikisha wanazinduka kutoka usingizini na kupata pointi tatu.
Mwambusi alisema wameiona Yanga katika mechi nyingi alichofanya ni kuwaelekeza wachezaji mbinu bora ambazo zitawapa ushindi na kwa maandalizi waliyofanya anaamini lengo lao litatimia.
Mwambusi anaingia kwenye mchezo wa leo tumaini lake likiwa kwa washambuliaji wake, Obrey Chirwa aliyewahi kucheza Yanga viungo Papy Tshishimbi na Never Tiger ambao wamekuwa na mchango mkubwa kwenye timu hiyo iliyorejea Ligi Kuu msimu huu.