DAR ES SALAAM; Mtaani hivi sasa mashabiki wa klabu za Simba na Yanga wameanza kujadili kuhusu usajili wa wachezaji mbalimbali kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara na michuano ya kimataifa na miongoni mwa wachezaji hao ni Mzambia Clatous Chama wa Simba.
Wapo baadhi ya mashabiki wa Yanga wameanza kuwakoga wenzao wa Simba wakiwaambia Chama maarufu kama Mwamba wa Lusaka mwakani atapatikana pale klabu ya Yanga makutano ya Mitaa ya Twiga na Jangwani, Dar es Salaam, hivyo Simba waanze kujiandaa kisaikolojia.
Ikufikie kuwa wakati vijiweni huko mashabiki wanatishana, hali ni tofauti ndani ya Yanga, ambapo Meneja wa timu hiyo, Walter Harrison anasema hizo ni tetesi tu za mitandaoni wenyewe hawajawahi kukaa mezani kujadili kuhusu kumsajili Chama ambaye mkataba wake Simba unaelekea ukingoni.
Akizungumza na HabariLEO , Walter amesema hakuna taarifa rasmi za Yanga kumtaka Chama hivyo zinabakia kuwa tetesi za mitandaoni.
“Hayo ni maneno ambayo yanazungumzwa katika mitandao ni kitu cha kawaida, lakini hakuna kitu chochote rasmi ambacho uongozi wa Yanga umeshakizungumza,”amesema Walter.