YANGA imetanguliza mguu mmoja mbele kuelekea hatua ya nusu fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya jana kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 katika mchezo huo uliochezwa Uyo Nigeria.
Kwa ushindi huo Yanga itahitaji sare ama ushindi wa aina yoyote kusonga mbele na kwa Rivers United ambayo wiki moja inayokuja watakuwa ugenini watahitaji kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 kusonga mbele.
Aidha, ushindi huo wa Yanga ni kama kisasi kwani msimu uliopita wakiwa nyumbani kwao Nigeria, Rivers United waliifunga Yanga bao 1-0 ikiwa ni baada ya kutoka ushindi kama huo kwenye mchezo wa raundi ya awali uliochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Mabao yote mawili ya Yanga katika mchezo huo uliopigwa katika dimba la Godswill Akpabio uliopo kwenye Mji wa Uyo, Nigeria yalifungwa kipindi cha pili na mshambuliaji Fiston Mayele katika dakika za 74 na 81 akizitendea haki pasi za nahodha Bakari Mwamnyeto na kumfanya mfumania nyavu huyo kufikisha mabao matano kuanzia hatua ya makundi ya michuano hiyo.
Kipindi cha kwanza ilishuhudiwa timu hizo zikienda mapumziko bila kufungana huku wenyeji Rivers United wakiutawala mchezo na kufanya mashambulizi mengi ambayo yaliokolewa na walinzi wa Yanga, wakati Yanga nao katika kipindi hicho walipata nafasi tatu za mabao lakini Aziz KI, Farid Mussa na Mudathir Yahya walishindwa kuzitumia.
Kipindi cha pili Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi alikianza kwa kufanya mabadiliko matatu kwa pamoja ambapo aliwatoa Djuma Shabani, Joyce Lomalisa na Farid Mussa nafasi zao zikachukuliwa na Tuisila Kisinda, Jesus Moloko na Kibwana Shomari.
Mabadiliko hayo yaliiongezea nguvu Yanga na kuanza kufanya mashambulizi mengi kwenye lango la Rivers United mpaka kufanikiwa kupata mabao hayo mawili ambayo yaliwavunja nguvu wenyeji wao na kujikuta wakitoka uwanjani vichwa chini.
Comments are closed.