Yanga yaiendea Polisi kambini

KOCHA msaidizi wa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Yanga, Cedric Kaze amesema kikosi cha timu hiyo kinaingia kambini leo kujiandaa na mchezo wake wa Ligi Kuu dhidi ya Polisi Tanzania keshokutwa.

Yanga inashuka kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kuikabili Polisi ikiwa na kumbukumbu nzuri ya kushinda mchezo wa mzunguko wa kwanza kwa mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha.

Yanga iko kileleni mwa msimamo ikiwa na pointi 38 ikishuka uwanjani mara 15 ikishinda michezo 11 sare tatu na kupoteza mara moja.

Akizungumza na HabariLEO jana, Kocha Kaze alisema malengo yao ni kukusanya pointi kila mechi ili kuendelea na kampeni yao ya kupata matokeo mazuri katika michezo iliyopo mbele yao  katika kufanikisha mbio za kutetea taji lao.

“Lengo letu ni kutetea makombe yetu ambayo tulishinda msimu uliopita, hilo litatimia iwapo tutashinda kila mchezo ulio mbele yetu kwani mzunguko wa pili mara nyingi umekuwa mgumu,” alisema Kaze.

Alisema hawatawadharau wapinzani wao kwani hakuna timu rahisi kwenye Ligi Kuu Bara hivyo watawaheshimu Polisi Tanzania licha ya kuwa wako mkiani mwa msimamo.

Habari Zifananazo

Back to top button