DAR ES SALAAM; Yanga imezindua kitabu chake cha historia ya klabu hiyo, kiitwacho Klabu Yetu, Historia Yetu, huku ikiimwagia sifa Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) kutokana na maktaba ya kampuni hiyo kufanikisha mambo muhimu katika kuandaliwa kwa kitabu hicho.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, usiku wa kuamkia leo wakati wa uzinduzi wa kitabu hicho, ambapo mgeni rasmi alikuwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Dotto Biteko, Rais wa Yanga, Hersi Said, amesema wanaishukuru TSN kwa kupata baadhi ya vitu muhimu vilivyosaidia kukamilika kwa kitabu hicho.
“Maktaba ya TSN imekuwa msaada mkubwa kufanikisha kuandaliwa kwa kitabu chetu,” amesema na kuongeza kuwa kutokana na hali hiyo Yanga imetoa cheti maalumu cha shukurani kwa kitendo hicho cha TSN.
Kampuni ya TSN ni wachapishaji wa magazeti ya Daily News, Sunday News, HabariLEO na pia inaendesha mitandao ya kijamii ya magazeti hayo, pamoja na Youtube chaneli.
Kauli kama hiyo pia ilizungumzwa na Mwenyekiti wa jopo la wahariri walioandaa kitabu hicho, Mudhihir Mudhihir aliyesema kuwa TSN pamoja na Kampuni ya Uhuru Media Group(UMG) na Mwananchi Communication (MCL), zimefanikisha kwa kiasi kikubwa kukamilika kwa kitabu hicho.
Licha ya Mudhihir wengine walioandaa kitabu hicho ni Theophil Makunga, Joseph Kulangwa, Amir Mhando, William Shao na James Nhende.