Yanga yaingia mkataba na Jackson Group

KLABU ya soka ya Yanga imeingia makubaliano ya ubia wa kimasoko na Kampuni ya Jackson Group kwa miaka miwili kwa ajili ya kutafutiwa fursa za kibiashara, wadhamini kwa maendeleo ya timu hiyo.

Akizungumza jana Rais wa klabu hiyo, Hersi Said alisema kampuni hiyo inakwenda kufungua milango kwa wadau kuwasaidia kusonga mbele kimaendeleo kwani klabu hiyo ina mpango wa kuwa na miradi mingi inayohitaji ushirikiano.

Alisema kampuni hiyo inajihusisha na uwakala wa masoko nchini Tanzania na huduma mbalimbali ikiwa ni pamoja na usimamizi wa haki za biashara, kufanya kazi na wadau wanaojihusisha na udhamini kwenye michezo wakiwa na uzoefu mkubwa wa kufanya kazi na wadhamini wa ndani, Afrika na Ulaya.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Jackson Group, Kelvin Twissa alisema anafurahi kufanya kazi na timu kubwa kwani uzoefu wao wa ndani na wa kimataifa utasaidia Yanga kurudisha thamani ya uwekezaji na kuwaweka katika kiwango kipya.

“Sababu ya kuwepo Yanga tuna uzoefu na tumefanya kazi kwenye taasisi mbalimbali za ndani na nje ya nchi, tuliyojifunza huko tunaamini tutaisaidia klabu hii kufikia malengo kwa kupata watu wa kufanya nao kazi ilimradi haki za kibiashara zizingatiwe,” alisema.

Alisema wameamua kufanya kazi na Yanga kwa sababu wanaamini sio watu wa kushindwa, wana utawala bora na wanalinda haki za biashara na kwamba timu hiyo anaamini atakuwa ni mdau mzuri katika makubaliano yao.

“Kazi yetu ni kuiuza Yanga kwa wadau, kutafuta wadhamini, kutafuta fursa za fedha ili kuleta tija, thamani ya klabu kupanda kwa kiwango cha juu,” alisema.

Habari Zifananazo

Back to top button